Amemkatisha Mtoto Kunyonya Kwa Ajili Ya Kwenda Kutafuta Elimu - Je, Amlipe Mtoto?

SWALI:

 

Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

Sifa zote njema anastahiki kushukuriwa Allah Subhanahu Wata'ala.

Mimi ni mama mwenye mtoto wa kiume ambae nilimkatisha kunyonya kwa ajili ya kuondoka ndani ya nchi na kwenda nchi nyengine kwa kwenda kutafuta Elimu.

 

Nilikuwa nina nia ya kumchukuwa mtoto wangu huyo lakini kutokana na mazingira ya nchi niendayo ikaniwia vigumu kumchukuwa, kwani sikuwa na mtu wa kuweza kukaa nae pindipo nitakapo ingia darasani. Nilimuacha akiwa na umri wa mwaka mmoja na mwezi mmoja, naomba kufahamishwa ni kweli utakapomkatisha maziwa mtoto unatakiwa umlipe na ni vipi naweza kumlipa?

 

InshaAllah nawatakia kila la kheri

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumuachisha mtoto wako kunyonya.

Ni jambo linalofahamika vyema kabisa sasa kuwa maziwa ya mama ndio mazuri sana kwa siha, afya na makuzi mazuri kwa mtoto. Kwa hiyo, Allaah Aliyetukuka Amewaagizia kinamama wawe ni wenye kuwanyonyesha watoto wao miaka miwili kamili. Hata hivyo, hilo ni kwa atakayetaka kukamilisha muda huo, (al-Baqarah [2]: 233).

 

Pia, wazazi (mama na baba) wanaweza kushauriana katika kumuachisha mtoto kunyonya kwa sababu moja au nyingine. Mashauriano hayo yawe ni yenye kutazama maslahi ya mama na mtoto. Kila mmoja asiwe ni mwenye kudhuriwa na mwengine kwa njia yoyote ile.

 

Ikiwa wazazi watashauriana kumuachisha mtoto kutakua hakuna kulipwa chochote mtoto. Kwa sababu ya mama kutokuwepo au kwa sababu nyingine yoyote ile ambayo itamfanya asiweze kumnyonyesha, jukumu la kumpatia mtoto mwangalizi au mnyonyeshaji mwengine litamuangukia baba. Baba atalazimika kumuajiri mwanamke wa kumnyonyesha mtoto au kumtazama.

 

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

 

Je Kuna Malipo Kama Hukumnyonyesha Mtoto?

 

Mama Hataki Kunyonyesha - Nini Hukmu Yake?

 

Mtoto Asiyenyonyeshwa Na Mama Yake Inapasa Alipwe?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share