Kisomo Cha Arubaini Baada Ya Maiti Kufa Ni Sunnah Au Bid'ah?

 

Kisomo Cha Arubaini Baada Ya Maiti Kufa Ni Sunnah Au Bid'ah?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Imezoeleka maiti anapozikwa baada ya siku tatu watu hufanya kisomo, wengine hufanya Arobaini  je hiki kisomo haswa kinahitajika kifanyike lini? na hii Arobaini inabidi iwe imesomwa kabla au baada ya kupita siku Arobaini tangu kupita mazishi?
 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Hakika ni kuwa jambo hili la kufanya kisomo baada ya siku tatu au kufanya arobaini na watu kula mpunga kama katika karamu ni mambo yaliyozoeleka sana. Zipo sehemu nyingine wanakusanyikana Msikitini kwa ajili ya kisomo kwa siku tatu mfululizo. Lakini kwa kuwa uchumi umezorota huwa siku hizi inafanywa siku moja peke yake na thawabu ya kisomo wanaona zinamfikia maiti.

 

Hakika jambo hili halikuthubutu kabisa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema. Hakika ni kuwa kisomo hicho thawabu zake hazimfikii maiti.

 

Ifahamike kuwa katika Uislamu hakuna kabisa mas-alah ya siku arobaini. Arobaini kimtazamo wa fiqhi ni zile siku  za uwingi ambazo anakaa mwanamke aliyezaa akiwa anatokwa na damu ya Nifaas. Wakati huu mwanamke huyo huwa ana udhuru hivyo haruhusiwi kishari’ah kuswali wala kufunga.

 

Sasa na watu wenye kupenda mambo ya kuzua mambo katika Dini bila msingi wowote wamechukuwa kuwa baada ya mtu kufa watu wanakusanyikana katika nyumba ya aliyefariki wakifanya kisomo na du’aa na hapo kuandaliwa chakula aina kadhaa ili watu wale pamoja na kumkumbuka aliyefariki. Hakika jambo hili la arobaini halipo kabisa na hivyo ni uzushi.

 

Inabidi sisi tuachane na jambo hilo na tuangalie mambo ambayo yanaweza kumfaa maiti kaburini. Yapo mambo mengi lau yatafanywa na watu wa aliyefariki basi yeye anapata thawabu japokuwa keshafariki. Miongoni mwa mambo hayo ni:

 

1.     Kuombewa Du’aa na mtoto wake mwema.

 

2.     Kulipiwa madeni anayodaiwa.

 

3.     Kufanyiwa Hajj ikiwa hakuwahi kufanya.

 

4.     Kutolewa sadaka wakati wowote ule na sio baada ya   siku arobaini au siku tatu.

 

5.     Kumlipia nadhiri zake.

 

6.     Waislamu kwa jumla kumuombea Du’aa.

 

Hayo ni mambo yatakayomsaidia sana kuliko mkusanyiko wa mara moja na watu kusoma, kula na kuondoka.

 

Kadhaalika soma makatazo ya jambo hilo kwenye kitabu cha ‘Bid-a’ cha Shaykh ‘Abdullaah Swaalih Farsiy, ambacho vilevile kinapatikana hapa:

 

Bid'ah - Shaykh 'Abdullaah Swaalih Faarsiy (Aliyekuwa Qaadhi Wa Zanzibar Na Kenya)

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi 

 

 

Share