Mashairi: Mume Bora

                    Mume Bora

 

                      ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

Alhidaaya.com

               

 

 

Salaamu zangu natuma, zifike kila mahali,

Tunaziomba rehema, za Mola zituwasili, 

Hapo siku ya Qiyaama, tuwe chini ya kivuli,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Akiposa Muumini, huyo mume mkubali,

Mume aloshika dini, na kila siku huswali,

Mwenye akili kichwani, usikudanganye mwili,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Usitafute uzuri, au yule mwenye mali,

Chagua tabia nzuri, alotulia akili,

Aloleleka vizuri, kidini na kiasili,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Mume yule mwenye kazi, na mwenye mustaqbali,

Sio mvivu wa kazi, mpuuzi asiejali,

Awe anafanya kazi, yenye mali ya halali,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Awe mume wa huruma, hapana yule katili,

Awe ni mwenye heshima, sio jeuri jahili,

Awe ni mwenye hekima, mwenye busara kamili,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Tafuta mume haraka, na kwa Mola tawakali,

Ikufikie baraka, ya Mola Wako Jalali,

Utulie kwa hakika, tabia mbaya badili,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Fadhila zake ni nyingi, uliza kila pahali,

Huo ndio ni msingi, wa maisha ya halali,

Ni kinga kwa mambo mengi, kwa madhambi mbalimbali,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Kuolewa ni utulivu, tumeshaona dalili,

Huyaondoa maovu, na mambo huwa sahali,

Hukufanya mtulivu, shida ikikukabili,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Wajibu wako timiza, nyumbani mpo wawili,

Mkikaa kuzungumza, na mambo kuyajadili,

Mjaribu kueleza, muelezane ukweli,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Mume ni msimamizi, kwa mali na kila hali,

Ayaonyeshe mapenzi, maneno kama asali,

Katika masimulizi, asiseme kwa ukali,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Mola awape watoto, hao ni rasilmali,

Mke ni mama watoto, awe mwema na mkali,

Awatazame watoto, wasikuwe kijahili,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Mke ni nguzo nyumbani, kama vile matofali,

Na mume ndio rubani, huona yaliyo mbali,

Kamba ya Mola shikeni, ibada iwe awali,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

Mola Watunze vigoli, pamoja na wanawali,

Wawe kama wa awali, kama zama za Rasuli,

Nimemaliza kauli, hapa nafunga kufuli,

Akiposa mkubali, mume bora Muumini.

 

 

 

 

Share