Dhul-Hijjah: Inafaa Kulipa Deni La Ramadhwaan Pamoja Na Niyyah Ya Swawm Za Naawafil Kama Dhul-Hijjah?

 

Inafaa Kulipa Deni La Ramadhwaan Pamoja Na Niyyah Ya Swawm

 Za Naawafil (Sunnah) Kama Dhul-Hijjah?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Je inafaa kutia nia mbili ya kufunga Sunnah kama siku za dhul-hijja,  na kulipa deni la Ramadhani?

 

 

JIBU: 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kutokana na Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya niiyah na ile ya Swawm za sita za Shawwaal, wanaonelea kuwa Swawm zozote za Sunnah zikichanganywa niyyah moja na Swawm za deni basi mtu anatarajiwa kupata ujira wa zote isipokuwa tu Swawm ya deni kuchanganywa na Swawm ya sita ya Shawwaal pekee ndio haiwezi kulipwa kwa niyyah moja kwani Hadiyth inaonyesha wazi kuwa mtu anatakiwa akamilishe Swawm ya Ramadhwaan ndio afunge sita za Shawwaal ili aweze kupata ujira uliotajwa katika Hadiyth isemayo:

 

((من صام رمضان ثم أتبعه بست من شوال))

Atakayefunga Ramadhwaan, kisha akafuatia na Sita za Shawwaal ni sawa na aliyefunga mwaka mzima

[Muslim, Abuu Daawuwd, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad na ad-Daarimiy].

 

Kiunganisho cha neno 'kisha' katika Hadiyth hiyo kinaonyesha kuwa kufunga huko lazima kutimizwe kwa mpango, yaani kwanza kukamilisha Swawm ya Ramadhwaan pamoja na deni lakekama mtu analo, kisha kufunga Sitta Shawwaal ili kupata hizo fadhila zilizotajwa katika Hadiyth.  Aliyefunga Ramadhwaan bila ya kuikamilisha hatambuliki kuwa ni yule aliyetajwa kupata hizo fadhila za kufunga mwaka mzima.

 

Kwa hiyo kutia niyyah moja katika Swawm hii ya Sitta Shawwaal haiwezekani, bali ikiwa  atafunga mtu deni lake katika siku za kufunga Sunnah yoyote nyingine kama Jumatatu na Alkhamiys, au siku za Ayaamul-Biydhw (tarehe 13, 14, 15 za Kiislam), au siku ya 'Aashuraa au 'Arafah  ndio inawezekana kutia niyyah pamoja na Swawm hizo na huweza kupata thawabu za fadhila zote.  

 

Inakubalika kulipa deni la Ramadhwaan pamoja na kufunga siku za mwanzo za Dhul-Hijjah kwa sharti kwamba niyyah iwe kwanza ni ya kulipa deni la fardhi kwa sababu hilo ndilo muhimu zaidi kutimizwa kabla ya Swawm ya Naafil (Sunnah). Na Rehma ya Allaah ni pana sana hivyo utakapotia niyyah ya kulipa deni na kufunga Swawm katika siku hizi tukufu kwa ajili ya kupata fadhila zake pia, utapata thawabu zote mbili In Shaa Allaah kwani kila jambo linategemea niyyah yake kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى))  متفق

“Vitendo vinategemea (vinalipwa kwa) Niyyah na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokusudia.”  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na hata kama hukupata thawabu za kufunga Nawaafil (Sunnah), utakuwa umetimiza waajib wa kutekeleza fardhi na umeshajitoa katika jukumu lake, kwani kukosa kutimiza fardhi bila ya sababu ziloruhusu ki-sharyi’ah huwa ni dhambi.

 

Jambo lisilopasa ni kuunga nia mbili ya kulipa deni la Ramadhwaan na Swawm ya Sitta Shawwaal kwani haya ni mas-ala mahsusi ambayo inatofautiana na Swawm  nyinginezo kutokana na dalili zake ambazo maelezo yamo katika maswali na majibu yafutayo:

 

Inafaa Kutia Niyyah Mbili Ya Kulipa Swawm Na Sitta Shawwaal?

 

Kulipa Deni Kwanza Au Kufunga Sitta Shawwaal

 

Kulipa Deni Mwanzo Au Kufunga Sitta Shawwaal? Je, Inafaa Kulipa Jumatatu Na Alkhamiys?

 

Kulipa Deni La Ramadhaan Na Sitta Shawwaal

 

Kulipa Deni Mwanzo Au Kufunga Sitta?

 

Ufafanuzi Wa Thawabu Za Sitta Kama Kufunga Mwaka Mzima

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share