Sitta Shawwaal: Inafaa Kutia Niyyah Mbili Za Kulipa Deni La Ramadhwaan Na Sita Shawwaal?

 

Inafaa Kutia Niyyah Mbili Za Kulipa Deni La Ramadhwaan Na Sita Shawwaal?

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

As-salaam alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

Naomba fatwa kwa masuala yangu yafuatayo:
 
Je inawezekeana kwa mwanamke aliyeingia kwenye siku zake (hedhi) katika mwezi wa ramadhani, baada ya ramadhani kumalizika, kufunga ( kulipa ) ramadhani na wakati huo huo (sambamba) kufunga sitatul shawwal? yaani kama piriadi yake ni siku 5 na sitatul shawwal siku 6, akafunga siku 6 kwa kutia nia mbili pamoja?
a) kama inawezekana atatia nia vipi?
b) kama haiwezekani, ni funga ipi aianze kwanza ? yaani siku alizozikosa ramadhani au anaweza kuanza na sitatul shawwal, badae ndio akalipa ramadhani
 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Haiwezekani kufunga deni na Sita Shawwaal kwa niyyah moja.  Rai iliyosahihi ni kwamba, kufunga Sita Shawwaal kunawezekana tu baada ya kumaliza deni kwanza la Ramadhwaan. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

((من صام رمضان ثم أتبعه بست من شوال))

 

Atakayefunga Ramadhwaan, kisha akafuatia na Sita za Shawwal…

[Muslim, Abu Daawuwd, Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad, Ad-Daarimiy].

 

Kiunganisho cha neno 'kisha' katika Hadiyth hii ni dalili kuwa kufunga huko lazima kutimizwe kwa mpango, yaani kwanza kukamilisha funga ya Ramadhwaan pamoja na deni lake kama mtu analo, kisha ndio kufunga Sita Shawwaal ili kupata hizo fadhila zilizotajwa katika Hadiyth.  Aliyefunga Ramadhwaan bila ya kuikamilisha hatambuliki kuwa ni yule aliyefunga Ramadhwaan kamili.

 

Kwa hiyo kutia niyyah moja katika funga hii ya Sita Shawwaal haiwezekani, bali ikiwa  atafunga mtu deni lake katika siku za kufunga Sunnah yoyote kama Jumatatu na Alkhamiys, au siku za Ayaamul-Biydhw (tarehe 13, 14, 15), au siku ya 'Ashuraa au 'Arafah  ndio inawezekana kutia niyyah pamoja na Swawm hizo na huweza kupata thawabu za fadhila zote.  

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi: 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share