Mchumba Bado Hana Uwezo Kunioa, Je, Kuwasiliana Kabla Ya Ndoa Kunakubalika?

 

SWALI:

 

Mimi ni msichana mwenye miaka 22 ambae nipo chuo kwa sasa na bado sijabahatika kuolewa. Kipindi cha nyuma nilipendana na kijana mmoja ambaye lengo letu kuu ni kuoana, ila kutokana na mazingira pamoja na pirika za maisha imebidi asafiri kwenda nje kwa ajili ya kuhangaikia maisha. Kwa kipindi cha miaka kadhaa tumekuwa tukiwasiliana kwa simu na lengo letu likiwa ni lile lile. Lakini baada ya kusikiliza mawaidha fulani na kusoma sehemu mbali mbali tumegundua kwamba kitu tulichokuwa tukifanya ni makosa.

Kwa sababu si halali kwetu kuongea kimapenzi wakati hatujaoana. Tumejadili kuhusu hilo na tumeona ni vizuri kuomba msamaha kwa Allah (s.w). Lakini sote bado tuna nia nzuri na tumejua kosa letu. Tatizo lilokuwepo ni kwamba mimi bado nasoma na yeye bado hajajiweka sawa kimaisha. Je tufanyeje? Tunataka tufanye haraka kuoana, jee inafaa kuongea ikiwa maongezi ni ya kawaida au tusiongee mpaka atakapokuja nyumbani? Ahsante.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu maongezi kabla ya ndoa.

Mwanzo tuna furaha kuona kwamba Waislamu wanafuatilia mambo ya Dini yao. Na uzuri zaidi ni kuwa pindi wanapopata kuwa waliokuwa wakifanya ni makosa basi wanarudi nyuma na kuomba msamaha kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa makosa yaliyopita.

 

Hii inaonyesha Imani tuliyo nayo ya Dini yetu. Tufahamu kuwa Uislamu unapoweka maagizo ya kujiepusha na jambo basi huweka kuwa jambo lolote linaloweza kuwapelekeni katika dhambi nalo ni kosa. Ndio Allaah Aliyetukuka Hakusema msizini bali msikaribie zinaa. Hivyo, jambo lolote linalowaleta au kukuleta na zinaa limekatazwa kabisa na shari’ah ili watu wasiingie katika madhambi. Unaweza ukaona kuwa jambo hilo la kuzungumza tu ni la kawaida sana lakini madhara huenda yakaonekana baadaye ya mbali au karibu.

 

Jambo la nyinyi kufanya ni mume atume salamu za posa kwa wazazi wako, kupitia kwa wazazi wake au wazee wake wa karibu. Wazazi wako pamoja na wewe mwenyewe mnapokubali basi hapo kunapokuwa na dharura mnaweza kuzungumza na hata akija likizo anaweza kuja kwenu na kuzungumza nawe ukiwa umevaa vazi la heshima mbele ya Mahram yako, akiwa ni baba, mama, kaka, mjomba au ‘ami au mwengine yeyote ambaye hawezi kukuoa.

 

Kwa hiyo, hata hayo maongezi ya kawaida yawacheni kwa sasa ili kujihifadhi kutokana na dhambi lililo kubwa kwa njia moja au nyingine.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi

Mawasiliano Na Mchumba Baada Kuposa Na Kabla Ya Ndoa

 

Anaweza Kuzungumza Na Kuonana Na Aliyemposa?

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awafanyie sahali njia yenu ya kuoana na yawe masikilizano mnapoingia katika uanandoa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share