Inafaa Kutoa Pesa Msikitini Kwa Ajili Ya Kuwaombea Wazazi Waliofariki Du’aa?

 

SWALI:

 

Assalaam aleykum,

 

Swali langu lahusu kutoa sadaq kwa ajili ya kuwaombea wazazi waliofariki.

 

Nikipeleka pesa msikitini na kuwaambia ni kwa ajili ya kuwaombea wazizi dua hiyo itapokelewa?

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutoa pesa Msikitini kwa ajili ya kuombewa du’aa wazazi wako. Hili ni jambo geni katika Uislamu na limekuja kwa sababu ya watoto kutojua haki za wazazi wao. Jambo hilo halikufanyika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) wala watangu wema. Suala hili limekuja kwa sisi kutowajali wazazi wetu waliotulea kwa shida na kutekeleza wajibu wetu kwao baada ya kuaga dunia kwao.

 

Allaah Aliyetukuka Ametupatia njia muafaka kabisa bila ya kuingia katika shughuli zisizofaa. Anasema Aliyetukuka: “Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni” (al-Israa’ [17]: 24). Kwa hiyo, hapa Allaah Aliyetukuka Anatufundisha kuwa tunatakiwa sisi tuwaombee wazazi wetu wanapokufa na huko ni kutimiza wajibu wetu kwao. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) akatusisitizia hilo pale aliposema: “Pindi mwanadamu anapokufa amali zake zote hukatika isipokuwa kwa mambo matatu: … na mtoto mwema anayemuombea du’aa” (Muslim).

 

Hili la kuomba du’aa ni moja lakini yapo mengine mengine ya kumfanyia mzazi wako ili aendelee kupata thawabu wakati tayari amezikwa. Miongoni mwayo ni:

 

  1. Kupeleka misahafu Misikitini kwa niaba yake.
  2. Kufukua kisima ili watu wapate maji ya kunywa kwa niaba yake.
  3. Kumlipia deni la funga ikiwa anadaiwa.
  4. Ikiwa hakuwahi kwenda Hijjah nawe ushakwenda waweza kwenda kwa niaba yake.

 

Haya ndio tuyafanye na acha ya kupeleka pesa ili uombewe bali omba mwenyewe.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:  

 

‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu

 

 

 

Na Allaah anajua zaidi.

 

 

 

Share