Du’aa Ya كَنْزُ الْعَرْش - Kanzul-'Arsh (Ganjul-'Arsh) Ni Uzushi Wa Mashia Na Masufi

 

Du’aa Ya كَنْزُ الْعَرْش - Kanzul-'Arsh (Ganjul-'Arsh) Ni Uzushi Wa Mashia Na Masufi

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Kuna vijitabu vidogo vinauzwa na watu huku wengi wanaisoma dua hiyo inayojulikana kwa ‘ganjul-arsh’ je hii dua ni kweli ya bwana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Du'aa hii haijulikani kabisa katika vitabu vya Hadiyth. Na ni dhahiri ni du’aa ya uzushi kwa sababu ya muundo na mpangilio wake wa kauli na maana ya hiyo du’aa inatosheleza kutambulika kuwa ni uzushi anaozuliwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kadhalika hizi ni katika zile du’aa za kutungwa na baadhi ya Mashia na Masufi ambazo wao huziita ‘Nyiradi’. Nazo ni katika mikusanyiko ya du’aa na maneno yaliyokusanywa kwa wale ‘Muridu’ wa ki-Sufi wazisome na kuzirudia katika nyakati maalum na kwa muundo fulani na kwa idadi maalum inayojulikana kwao.

 

Kwa kifupi haifai kuchukua mfumo huo na du’aa kama hizo na adhkaar au nyiradi zilizotungwa na Mashia na Masufi au watu wowote na kuzifanyia kazi. Ni wazi kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Du’aa ni ‘Ibaadah" [Imepokewa na Abu Daawuud, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah. Na Imaam Al-Albaaniy kasema ni sahihi]. Na hivyo, maadam du’aa ni ‘Ibaadah, basi du’aa zetu tutazichukua kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kutoka katika Qur-aan.

 

Hapana shaka kwamba du’aa hiyo ya “Kanzul-‘Arsh” au “Ganjul-‘Arsh” kama wengine wanavyoiita, na yaliyonukuliwa humo kuhusu fadhila zake ni uzushi, achilia mbali kuwa ina mambo yanayokwenda kinyume na matini (nuswuus) za Dini (Qur-aan na Sunnah). Miongoni mwayo ni kumpa majina Allaah kwa majina yasiyothibiti katika Kitabu cha Allaah (Qur-aan) wala Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Mfano: Al-Burhaan (dalili). As-Swaafiy (halisi), Al-Mu’ujiz (Wa Miujiza), Al-Qadiym (Wa Kale), Al-Mukhlis (Anayetakasa wengineo), Al-Faadhil (Anayefadhilisha). Majina yote haya si miongoni mwa Majina Mazuri ya Allaah na Sifa Zake.

 

Imaam Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amefafanua mas-alah yanayojulisha kauli inapokuwa ni ya uzushi. Miongoni mwa tanbihi alizozitaja ni staili au aina ya uandishi mbaya wa maneno katika hizo zinazodaiwa kuwa ni Hadiyth, na vile ilivyo na kusikika katika masikio kuwa haikubaliki (haiingii akilini) katika sikio, na hali ya fitwrah (maumbile ya asili) ya binaadamu inaikanusha.

 

 

Hakika tuna duáa za kutosheleza kabisa katika kitabu cha Allaah (Qur-aan) na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilizothibiti kabisa. Na mtu anaweza kupata du’aa na adhkaar nyingi kwenye kitabu "Hiswnul-Muumin" au

 

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

kilichopo ndani ya Alihaadaya.com

 

na vyote vinapatikana kwenye maduka ya vitabu.

 

Na kwa hiyo hatuna haja ya kubadilisha badala yake kwa duáa uliyotaja katika swali. Imekuwa desturi sasa Waislamu wengi kuacha mafunzo yaliyothibiti kwa dalili na kushughulishwa na yale yasiyothibiti  na hivyo si chochote ila ni mvuto wa uovu.

 

Amesema Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah): “Hapana shaka kwamba adkhaar na du’aa ni ‘Ibaadah bora kabisa, na ‘Ibaadah ni jambo mojawapo ambalo hakuna upenyo wa mtu kuleta rai zake. Inatupasa tufuate aliyotufunza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na si hawaa na matamanio yetu au uzushi. Du’aa na adhkaar za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni bora zaidi kuliko zozote nyinginezo. Na mwenye kuzifuata atabakia salama na kutenda yaliyo sahihi, na manufaa na matokeo mazuri atakayochuma ni mengi hata hayaelezeki. Du’aa na adhkaar zozote nyinginezo zinakuwa ni haraam, au makruuh kwani zinaweza kuhusiana na shirk japokuwa watu wengi hawatambui hilo. Maelezo yake ni marefu mno kuyaelezea hapa.

 

Mtu hana haki kufundisha watu du’aa au adhkaar zozote zisizokuwa katika Sunnah, au kuzifanya kuwa ni ‘Ibaadah ya mazoea ambayo anategema watu kuifanya kama wafanyavyo Swalah tano. Hii ni uzushi katika Dini ambao Allaah Hajautolea idhini. Ama kupanga uradi au kusoma kwa kudumisha dhikri ambayo haikuamrishwa katika shari’ah, ni jambo lisiloruhusiwa. Du’aa na adhkaar ziloamrishwa katika shari’ah, ni bora zaidi kwa yeyote kuzitaraji na kuzipata na hakuna anayezipuuza kwa kufadhilisha zilizo mpya za uzushi, au adhkaar za uzushi isipokuwa ambaye ni mjinga au mtendaji makosa.”

 

[Majmuu’ Al-Fataawa 22/510/511]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share