Mchuzi Wa Kuku Na Mchicha

Mchuzi Wa Kuku Na Mchicha

  

Vipimo 

Kuku - 1 au pound 4 

Vitunguu maji -  5  

Nyanya/tungule -   3 

Nyanya kopo (tomatoe paste) -   4 vijiko vya supu 

Mchicha - 2 misongo (bunch)  

Tangawizi mbichi ilosagwa - 1 kijiko cha supu 

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa -  1 kijiko cha supu 

Pilipili mbichi ilosagwa - 1 kijiko cha chai 

Mafuta -  ½ kikombe 

Bizari ya mchuzi -  1 kijiko cha chai 

Bizari ya Methi/uwatu -  ½ kijiko cha chai 

Chumvi -  kiasi 

Ndimu -  1 moja kamua

 

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika 

  1. Mkate kuku vipande vya kiasi, msafishe na mwoshe vizuri weka kando. 
  2. Katakakata vitunguu, nyanya/tungule (chopped) weka kando. 
  3. Osha mchicha kisha  katakata weka kando. 
  4. Weka mafuta katika sufuria kisha kaanga vitunguu hadi viwe vyekundu kukaribia rangi ya brauni ilokoza.  
  5. Tia tangawizi ilosagwa pamoja na kitunguu thomu, tia bizari zote, kaanga kidogo tu. 
  6. Tia vipande vya kuku, kaanga ukigeuza huku na kule kwa muda wa dakika 5 takriban. 
  7. Tia nyanya/tungule na nyanya kopo kaanga kidogo tena, kisha tia maji ya kutosha kuku aive. Acha kwenye moto itokote/ichemke. 
  8. Tia pilipili mbichi ilosagwa pamoja na ndimu na chumvi.  
  9. Mwishowe karibu na kuku kuiva tia mchicha uchemke kidogo   Epua ukiwa tayari kuliwa na wali au mkate upendao. 

                     

Kidokezo: 

Ni vyema kumsafisha kuku kwa haldi/tumeric/bizari ya manjano au siki ili kukata harufu ya kidusi cha kuku.

 

 

 

 

 

 

Share