Quesadilla (Kay-sa-dee-yya) Ya Kuku, Pilipili Boga Na Vitunguu (Spanish)

Quesadilla  (Kay-sa-dee-yya)  Ya Kuku, Pilipili Boga Na Vitunguu (Spanish)

Vipimo

Mikate ya Tortillas - 15 takriban

Nyama kuku bila mifupa (kidari/breast)Osha, katakata vipande vipande - 2 Pounds (1 kilo takriban)

Vitunguu (rangi ya zambarau)Katakakata vipande (diced) – 2

Pilipili boga la kijani (capsicum)Katakata vipande (diced) – 1

Nyanya/tungule Katakata vipande (diced) – 2

Tangawizi mbichi Chuna (grate) - 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) Chuna (grate) - 1 kijiko cha supu

Pilipili manga - 1 kijiko cha chai

Mdalasini - 1 kijiko cha chai

Ndimu Kamua – 2

Chumvi – Kiasi

Jibini/cheese ya cheddar au marble Chuna (grate) - 500 gms

Samli - 4-5 vijiko vya supu

Kitoleo/Salsa Ya tayari dukani au tengeneza mwenyewe nyumbani upendayo. Au tumia malai machungu

(sour cream) - 1 kikombe

Namna Ya Kupika:

  1. Weka kuku katika sufuria. Kamulia ndimu, tia chumvi, pilipilimanga, mdalasini, kitunguu thomu na tangawizi mbichi.
  2. Funika apikike kwa maji yake na ya ndimu. Ikibidi, tia maji kidogo tu kiasi cha kuivisha.
  3. Akikakuka, epua tia katika mashine (chopper) asagike kidogo, au katakata vipande virefu refu na vidogodogo kiasi. Weka katika bakuli kubwa kiasi.
  4. Tia vitunguu, nyanya/tungule, pilipili boga, katika kuku uchanganye vizuri.
  5. Weka kikaangio (frying pan) katika moto wa kiasi paka samli kidogo.
  6. Katika sahani kubwa, weka mkate mmoja wa Tortilla, tia mchanganyiko wa kuku kiasi vijiko 2 vya supu.
  7. Nyunyizia jibini ilokunwa kisha funika kwa mkate mwingine wa Tortilla.
  8. Hamisha mkate wa Tortilla weka kwenda kikaangio kisha fanya kama kuukaanga kama unavyopika chapati na kugeuza upande wa pili pia hadi uwe rangi ya dhahabu-brauni (golden-brown).
  9. Epua weka katika sahani. Kata nusu ya mkate au kata mara nne iwe robo yake.
  10. Kula motomoto kwa kutolea na salsa ukipenda au malai machungu (sour cream) utakayoiweka katika kibakuli kidogo.

Kidokezo:

Tortilla (Mikate ya ki-Spanish) inauzwa tayari madukani. Unaweza kufanya chapati kavu na nyepesi kabisa badala yake.

Bonyeza kiungo kifuatacho kupata picha ya mikate ya Tortilla:

Quesadilla Ya Kuku Na Uyoga (Spanish)

Salsa inauzwa tayari au tengeneza mwenyewe sosi yoyote ya nyanya/tungule upendayo. Lakini ukipenda unaweza kuila quesadilla bila ya sosi kwani pia tamu mno!

 

Share