Kumbukumbu Ya Kifo (Death Anniversary) Nini Hukmu Yake?

 

Kumbukumbu Ya Kifo (Death Anniversary) Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 

Assalam alaikum warahmatullahi wabarakatuh

 

Shukrani sana kwa kazi mnayo ifanya kwakutuelimisha, Allah Awajaze kheri (Allahumma Amin)

 

swali langu, ni kwamba, nilifiliwa na baba yangu, nikasema(moyoni bila kutamka kwa watu) kuwa nikiwa bado hai na ikafikia ile tariki aliyofia baba yangu, (yani kila mwaka), nitakuwa nikifunga siku 3(yani siku ya kabla, na siku ile aliyozikwa, na siku ya baada yake)mfano, kafariki tarehe 28(kwahio nitafunga toka tarehe 27,28 na 29)ili iwe ni siku maalum zakumuombea dua .

 

Nilifaanikiwa kufanya hivyo mara chache, ila badae sikurudi kutekeleza hayo kwakuwa, kuna mara ilikuwa inafkia sina udhu(niko katika HEDHI),hadi ikafkia nikaacha kabisa kufanya hivyo.  sasa naulizia, je hiyo ni nadhiri? na kama sikuitekeleza kama nilivyosema je napata dhambi?

 

Naombeni jibu kwa swali hilo -haya kila lakheri na watakieni

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza ni dhambi katika Uislamu kuweka kumbukumbu ya kifo inayojulikana kama ni ‘death anniversary’. Hili ni jambo la kuiga makafiri ambalo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amekemea. Kwa hiyo kulitenda ni miongoni mwa madhambi makubwa unapaswa ujiepushe nalo kabisa.

 

 

Shariy’ah ya Kiislamu kuhusu mtu anapoweka nadhiri kwa ajili ya jambo lisilofaa basi anatakiwa asitekeleze hiyo nadhiri bali ajiepushe na hilo jambo. Dalili ni Hadiyth ifuatayo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أبي طريفٍ عَدِيَّ بْنَ حَاتِمٍ  الطَّائي (رضي الله عنه) قال: سَمِعْتُ رسول اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم) يَقُولُ: ((مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ ثُمَّ رَأَى أَتْقَى لِلَّهِ مِنْهَا فَلْيَأْتِ التَّقْوَى))  رواه مسلم  

Imepokelewa kutoka kwa Abu Twariyf ‘Adiyy bin Haatim (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nimesikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Atakayeapa yamini [kufanya jambo] kisha akaona linalomridhisha zaidi Allaah kuliko aliloliapia, basi amche Allaah kwa kufanya linalomridhisha Allaah)) [Muslim]

 

 

Kwa hiyo ukipenda kumfanyia wema mzazi wako aliyefariki unaweza kumfanyia mambo yaliyothibiti kutendwa. Nayo yanapatikana pamoja na dalili zake katika viungo vifuatavyo:

 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:  

 

‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu

 

 

Hayo ndiyo pekee yatakayomfaa mzazi aliyefariki. Ama mengineyo yanayotendwa katika jamii kama khitmah, matanga na arubaini ya kifo, yote haya hayakuthibiti kwa hiyo kutekelezwa kwake hayamnufaishi lolote maiti bali mtendaji anaingia katika dhambi na khasara ya kupoteza mali na wakati wake kwa amali isiyokuwa na thamani yoyote mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kama alivyosimulia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

 من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد  البخاري

Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika Dini yetu) basi kitarudishwa [Al-Bukhaariy]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share