Imaam Ibn Baaz: Hukmu Ya Nadharia Ya Mageuzi Ya Kidarwini (Darwnism) Wana-Aadam Wametokana Na Nyani?

Hukmu Ya Nadharia Ya Mageuzi Ya Kidarwini (Darwnism)

Je, Wana Aadam Wametokana Na Nyani?

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

www.alhidaaya.com

 

 

Nadharia ya Mageuzi (Darwinism) inapingana na Qur-aan na Sunnah na Ijmaa’.

Dai la kwamba mwana Aadam ametokana na nyani ni la uongo.

 

 

SWALI:

 

Nimesoma sana kuhusu dhana ya mwana Aadam kugeuka kutokana na mfano wa kizazi cha nyani. Nadharia hiyo inafundisha kwamba mwana Aadam amepitia ngazi tofauti hadi kufikia kuwa mwana Aadam anayeonekana hivi leo. Je, hili ni kweli? Je, viungo vya nyani ni sawa na vile vya mwana Aadam? Tafadhali tushauri juu ya hili, Allaah Akupatie ujira ulio bora kabisa!

 

 

JIBU:

 

Tamko hili ni la uongo, potofu, na linapingana na Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na halikadhalika kwa Ijmaa’ (makubaliano) ya Salaf (watangu wema waliopita).

 

Nadharia hiyo iliyoasisiwa na Darwin imethibitishwa kuwa ni ya uongo, kwani mwana Aadam wa leo asili yao imetokana na kizazi cha mwana Aadam, na wala si kutokana na nyani au kitu chengine chochote.

 

Allaah Amemuumba baba yetu Aadam (‘Alayhis-Salaam) kutokana na udongo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Kwa yakini Tumemuumba mwana Aadam kutokana na mchujo safi wa udongo”. [Al-Muuminuwn: 12]

 

Allaah Amemuumba Aadam kutokana na udongo na kufinyanga katika sura yake. Aadam alikuwa ni mrefu kwa vipimo sitini vya mkono, lakini watu wamekuwa wanapungua kimo tokea hapo kale. Ameumbwa kutokana na mfumo na umbo la mwana Aadam wa leo. Watoto wake waliumbwa kwa sura yake; wana masikio, macho, akili, na umbo sawa na la mwana Aadam wa leo. Wanasimama wima, wanazungumza, wanasikia na kuona, na wanaweza kutumia mikono yao.

 

Hawana mifumo ya kinyani na wala hawashabihiani na viungo vya nyani. Mwana Aadam ni viumbe vyenye asili ya kipekee kama walivyo nyani, nguruwe, mbwa, punda, paka, na kadhalika.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Na hakuna kiumbe chochote kinachotembea katika ardhi na wala ndege anayeruka kwa mbawa zake mbili, isipokuwa ni umati mfano wenu. Hatukusuru katika Kitabu kitu chochote. Kisha kwa Rabb wao watakusanywa”. [Al-An’aam:38]

 

Jamii hizi za wanyama zitakusanywa Siku ya Kufufuliwa ili kusawazishwa alama zao na itasemwa juu yao, ‘Kuwa vumbi’. Kwa upande mwengine, jini na mwana Aadam wataitwa kuwajibika na watalipwa kwa mujibu wa matendo yao; yeyote aliyemtii Allaah ataingia Jannah (Peponi) na yeyote aliyemkufuru Yeye ataingia Jahannam (Motoni).

 

Jamii hizi ni tofauti kabisa na jamii za wanyama; nyani wapo kwenye aina ambayo ina asili, mfumo na tabia za kipekee, na vivyo hivyo kwa nguruwe, mbwa, punda, ngamia, ng’ombe, mbuzi, na kadhalika. Kila aina hii ya mnyama ina umbo na tabia zake tofauti ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameziumba.

 

Yeye Ndiye Mwenye Hikmah na Mwenye Ujuzi wa kila linalotendeka na uumbaji wa kila mnyama. Waja wa Allaah ni lazima waamini kwamba uumbaji wa Aadam unatofautiana kabisa kutokana na uumbaji wa nyani; na mfumo wa Aadam upo sawa hadi leo na wala haunasibiani na nyani au kitu chengine chochote.

 

Dai la kwamba mwana Aadam amegeuka kutokana na mfano wa kizazi cha nyani litabakia kuwa ni batili na halikubaliki. Hivyo, ni sahihi kufahamu kwamba yeyote anayekubali nadharia hii ni Kafiri. Dhana sahihi kabisa ni kwamba yeyote anayeamini nadharia hii hali ya kuwa anafahamu kanuni ya Shariy’ah juu ya hili ni Kafiri na mtu huyo amemsingizia uongo Allaah, Rasuli wa Allaah na Qur-aan ambayo inatoa ufafanuzi ulio wazi wa uumbaji wa Aadam.

 

 

[Fataawa Nuur ‘Alaa Ad-Darb, juzuu ya 1, Mlango wa ‘Aqiydah, Mlango Kuhusiana Na Mada Zinazofanana Na Tawhiyd, Kudai Kwamba Wana Aadam Wamegeuka Kutokana Na nyani Ni Dai Batili. ]

 

Share