Imaam Ibn Baaz: Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa´ah Kwa Mukhtasari

 

 

 ‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa´ah   Kwa Mukhtasari

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

 

Nini ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa´ah?

 

 

JIBU:

 

 

‘Aqiydah (Itikadi) ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuamini kila alichokuja nacho Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  katika yale yaliyo na dalili katika Kitabu kitukufu cha Allaah nacho ni Qur-aan, na Sunnah za Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Ahlus-Sunnah wal-Jamaa´ah ni Maswahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yaani Muhaajiruwn na Answaar na wengineo katika Maswahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na Taabi´iyn waliokuja baada ya yao, na waliokuja baada ya Taabi´iyn na baada ya hao katika Maimaam wa Waislamu mpaka hivi leo. Wao ni wale wanaofuata  Manhaj ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakafuata Shariy´ah yake; kwa kauli, matendo na ´Aqiydah. Hawa ndio Ahlus-Sunnah wal-Jamaa´ah.

 

 

Wameitwa “Sunnah” kwa kushikamana kwao na Sunnah, na wameitwa Al-Jamaa´ah kwa sababu ya kufuata kwao haki, nao ni Maswahaba na ndio viongozi wao, kisha Taabi´iyn na waliokuja baada ya Taabi´iyn. Miongoni mwao ni Imaam mashuhuri Maalik (Rahimahu-Allaah) na Ash-Shaafi’iy naye ni mashuhuri, na Abuu Haniyfah, Ahmad bin Hanbal, Is-haaq bin Raahwyah, Al-Awzaa´iy, Ath-Thawriy na Maimaam wengineo na kama wao katika Maimaam wa Waislamu ambao wamethibitika katika njia ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakailingania na wakaitukuza na wakathibitika juu yake kwa kauli na matendo na ‘Aqiydah. Hao ndio Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah.   

 

 

Nao kwa sifa ya mukhtasari, ni wale ambao wameshikamana  na Kitabu cha Allaah kwa kauli na matendo na kwa Sunnah ya ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kauli na matendo na wakafuata Manhaj ya Maswahaba wa wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na waliowafuatia kwa ihsaan. Hao ndio Ahlus-Sunnah wal Jamaa’ah  ambao wameshikimana na yale aliyokuja nayo Al-Muswtwafaa ('Alayhisw-Swalaatu was-salaam)  kwa kauli na matendo  na ‘Aqiydah ya Majina ya Allaah na Swifa Zake na katika Tawhiyd Yake na kumsafishia Dini Yake na kutii amri za Allaah na Rasuli Wake na kuacha makatazo ya Allaah na Rasuli Wake.  Hao ndio Ahulus-Sunnah Wal-Jamaa’ah.

 

 

Wale wanaotumbukia katika maasi hawatolewi nje ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa´ah. Lakini ni juu ya mtu kuleta Tawbah. Ikiwa atatumbukia katika madhambi ya kuwaasi wazazi au kukata undugu au zinaa au maasi mengineyo kama hayo. Maasi hayo  hayamtoi nje ya Uislamu wala hayamtoi nje ya Ahlus-Sunnah. Lakini ni lazima alete Tawbah, atubie kwa Allaah na akimbilie Tawbah na ajute na aazimie kikweli kutokurudia  katika maasi. Hii ndio Madhehebu ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa´a kwamba mwenye kufanya maasi hatolewi nje ya Uislamu wala hakufurishwi, bali mtu huyo  huwa ni mwenye udhaifu wa iymaan inampasa atubie kikwelikweli kutokana na maovu aliyotumbukia  ambayo Allaah Ameyaharamisha, bila ya yeye kukufurishwa. Madhambi kama tulyotangulia kutaja; zinaa, wizi, kuasi wazazi wawli, kuapa kiapo cha uongo, kushuhudia uongo na maasi kama hayo. Haya yote yanapunguza iymaan na yanadhoofisha iymaan lakini Muislamu hatolewi nje ya uislamu wala hatolewi nje ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah.  Lakini lazima akimbile kutubia  na athibitike katika utiifu wa Allaah na kujuta yale maovu aliyopitia na kuazimia kikweli kutokurudi katika maovu baada ya kujitoa humo na kutahadhari nayo kwa kumuadhimisha Allaah na kumtii na kuwa na raghba ya kupata thawabu Zake na kutahadhari adhabu Zake Subhaanahu wa Ta’aalaa.  Na’aam

 

 

[Al-Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Ash-Shaykh Al-Imaam Ibn Baaz]

 

 

 

Share