Imaam Ibn Baaz: Vitabu Bora Kuhusu ‘Aqiydah

Vitabu Bora Kuhusu ‘Aqiydah

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Ni vitabu gani bora vya Kiislamu kwa wale wanaotaka kuimarisha Iymaan zao na ‘Aqiydah na (ili) kukutana na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akiwa Ameridhika nao?

 

 

JIBU:

 

Kitabu muhimu kuhusu ‘Aqiydah ni Qur-aan; ni kilicho na ukweli ulio wazi, Kitukufu na Kitabu adhimu. Kifanyie rejeo namna uwezavyo na kisome kila mara. Kina ‘Aqiydah, uongofu katika mema na makatazo dhidi ya maovu. Kama utakisoma kwa umakini, kwa shauku ya kujifunza na kufuata maelekezo yake kwa utulivu, ikiwa ni kwa maneno, vitendo au ‘Aqiydah, utaona mazuri yote ndani yake kuanzia mwanzo hadi mwisho, yaani kutoka Suwratul-Faatihah (Suwrah ya 1) hadi Suwratun-Naas (Suwrah ya 114):

 

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾

 

{Sema: “Najikinga na Rabb wa watu}. [An-Naas: 1]

 

Kama utakitafakari kitabu hichi tukufu na kukisoma kila mara, utaelewa ‘Aqiydah ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaikubali kutoka kwako na kutoka kwa Waumini.

 

Kisha, usome vitabu vya Hadiyth, kwa mfano Vitabu vya Swahiyh Mbili vya Hadiyth (yaani Al-Bukhaariy na Muslim) na vinginevyo.

 

Baada ya hapo, usome vitabu vya Wanachuoni maarufu kwa ‘ilm, uongofu na ‘Aqiydah sahihi, kama vile vitabu vilivyoandikwa na Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah, miongoni mwa hivyo ni:

 

Al-‘Aqydah Al-Wasitwiyyah

Al-‘Aqiydah At-Tadmuwriyyah

Al-‘Aqiydah Al-Hamawiyyah

Minhaaj As-Sunnah na

Majmuw’ Al-Fataawaa.

 

Pia kuna kitabu cha ‘Aqiydah kilichoandikwa na Ibn Abiy Zayd Al-Qayrawaaniy. Maelezo ya Ibn Abil-‘Izz kwa kitabu cha ‘Aqiydah Atw-Twahaawiyyah, ni miongoni mwa vitabu muhimu.

Kuna vitabu muhimu vya Ibn Al-Qayyim (Rahimahu Allaahu).

 

Pia kuna kitabu kilichoandikwa na Shaykh ‘Abdur-Rahmaan bin Hasan chenye jina la “Fat-hul-Majiyd” na vitabu vya Imaan vya Shaykh Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab:

 

Kitaab At-Tawhiyd,

Kashful-Shubhaat na

Thalaatul-Uswuul.

 

Pia kuna kitabu cha “Ad-Duraru As-Saniyyah” chenye Fataawa (hukmu za kishariy’ah zinayotolewa na Wanachuoni Waislamu wenye viwango vya juu) kilichotolewa na Wanachuoni wa Najd. Ninawashauri wanaoanza kutafuta ‘ilm waihifadhi Qur-aan kadiri wawezavyo, na kusoma vitabu vya:

 

At-Tawhiyd,

Kashful-Shubhaat na

Thalaatul-Uswuul.

 

Vitabu tajwa hapo juu vinaweka wazi ukweli wa sehemu tatu za Tawhiyd na Salafiyyah (Manhaj ya watangu wema), ambayo ni ‘Aqiydah iliyolinganiwa na Shaykh na Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhab (Rahimahu Allaahu), na ni ‘Aqiydah ambayo inatumika nchini Saudi Arabia. Kitabu hicho kinahusu kufuata Qur-aan na Sunnah, na kufuata Manhaj ya Salaf (watangu wema) kwenye ‘Aqiydah na hukumu kwa mujibu wa Qur-aan, Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mwenendo wa Swahaabah (Radhiya Allaahu ‘Anhum) na wafuasi wao.

 

Baadhi ya watu wanaiita ‘Aqiydah ya Kiwahabi, na wanafikiri kwamba ni ‘Aqiydah mpya iliyo kinyume ya Qur-aan na Sunnah. Hivyo sivyo; hii ni ‘Aqiydah iliyofuatwa na Salaf wa Ummah kama ilivyotajwa hapo kabla, lakini maadui zetu wameipa jina hili ili kuwafanya watu kuichukia na wengine kuwaiga wao (maadui zetu) kwa ujinga wao.

 

Hata hivyo, mtafutaji ‘ilm asikubali kudanganyika kwa suala hili; ni lazima waelewe ukweli kutoka katika vitabu vyao, na si kupitia madai ya maadui zao na wale wajinga wa ‘Aqiydah zao.

 

Allaah Atujaalie uongofu sote na mafanikio!

 

 

[Fatwa ya Ibn Baaz, Mjaladi wa 7, Hukmu ya kuunganisha makundi ya kidini]

 

Share