Imaam Ibn Baaz: Ni Nani Khawaarij; Je, Ni Makafiri Au Waislamu?

Ni Nani Khawaarij; Je, Ni Makafiri Au Waislamu?

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:

 

“Khawaarij ni kundi lenye ghuluw (kuchupa mipaka), lenye kujitahidi katika dini na lenye jitihada katika Swalaah na kusoma Qur-aan na yasiyokuwa hayo.

 

Wanawakufurisha wenye kufanya maasi kwa sababu ya uvukaji mipaka wao uliopita kikomo, wanaona mtu aliyezini kakufuru, aliyekunywa pombe kakufuru, asiyewatii wazazi wake kakufuru, wanakufurisha (Waislamu) kwa kufanya tu madhambi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewazungumzia (watu hao Makhawaarij) kwa kusema: “Litatoka kundi (katika dini) na kuangamia miongoni mwa Waislamu, mmoja wenu ataidharau Swalaah yake akilinganisha na Swalaah zao, na atakidharau kisomo chake (cha Qur-aan) akilinganisha na chao, (lakini pamoja na yote hayo ya kuonekana ‘Ibaadah zao kijuu juu ni kubwa) watatoka katika Uislamu kisha hawatorejea tena.”

 

Hao ndio Khawaarij ambao wana uchupaji, wanaposoma Qur-aan utavutika na kisomo chao, wanaposwali utavutika na Swalaah zao, lakini wana uchupaji mipaka katika kukufurisha watu. Wanamuona aliezini kakufuru, aliyekunywa pombe kakufuru, basi kwa sababu hizo akasema Nabiy Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Wanatoka katika Uislamu kama unavyotoka mshale na kupenya kwenye kiwindwa (na kutokeza upande wa pili), nikiwadiriki nitawaua kama walivyouawa watu wa ‘Aad. Kwa hivyo basi, mtakapowapata waueni, kwani kuwaua hao kuna malipo (siku ya Qiyaamah) kwa yule aliyewaua.”

 

Na Wanachuoni wengi wanaona kuwa hao (hukmu yao) ni waasi wazushi wapotofu, lakini hawawakufurishi. Usahihi ni kwamba wao ni Makafiri, kwa kauli yake (Nabiy): “wanatoka kwenye Uislamu na hawatorejea tena.” Hiyo ni dalili kwamba wao ni Makafiri. (Na kauli nyingine ya Nabiy): “Nikiwadiriki nitawaua kama walivyouliwa watu wa ‘Aad.” Na watu wa ‘Aad ni Makafiri.

 

Iliyo sahihi na dhahiri kutokana na dalili kwamba wao kwa uchupaji wao wa mipaka na kukufurisha kwao Waislamu, na kuwadumisha Motoni (wanadai wanaofanya maasi wakiingia Motoni hawatoki milele)…(hayo yanatosha kuthibitisha kuwa) wao ni Makafiri, kwa sababu wanamuona mtenda maasi ni Kafiri na ni mwenye kudumu Motoni, na huu ni upotofu wa mbali –Allaah Atukinge na Atuweke mbali- na huko ni kutoka kwenye duara la Uislamu – Allaah Atukinge na Atuweke mbali-.

 

Tunamuomba Allaah msamaha na afya.

 

 

[http://www.binbaz.org.sa/noor/11822]

 

 

Share