Khitmah Kutokufaa Na Madhara Yake

 

Imetayarishwa na Abu 'Abdillaah

 

 Alhidaaya.com

 

BismiLlaah Rahmaan Rahiim

 

 

Khitmah Ni Nini?

 

Khitmah kilugha ni kuihitimisha Qur-aan nzima; kuisoma Qur-aan kuanzia mwanzo wake surah namba moja yaani Suratul Faatihah (Alhamdu) hadi mwisho wake ambayo ni Suwrah namba 114 yaani Suwrah Naas (Qul A'udhu birabbin Naas).

 

Lakini imegeuzwa maana hiyo ya kilugha na kugeuka katika matumizi ya walioanzisha huo utaratibu wa kumsomea Maiti Qur-aan na kuita kisomo hicho cha kumsomea Maiti kuwa ni Khitmah kwa sababu ndani yake kuna kuisoma Qur-aan yote. Hukusanyana watu pahala; kwenye nyumba ya aliyefariki, au ukumbi wa kukodiwa au Msikitini na kugawana juzuu kila mmoja na husomwa hiyo Qur-aan kwa sauti na kila mmoja kwa utaratibu wake na bila hata kumalizika. Kadhaalika huchomwa ubani n.k. Na wasomao hutaraji thawabu ya kusoma kwao hiyo Qur-aan imfikie Maiti. Na mambo haya yalianza baada ya kupita vipindi vitukufu ambavyo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivisifu.

 

Baada ya taarifu hiyo, maswali yafuatayo yanamiminika:

 

1)   Watu wanaposoma Khitmah husoma Qur-aan na kusoma Qur-aan ni jambo zuri na la 'Ibaadah, sasa kwa nini isifae kuisoma kwenye Khitmah?

 

2)   Je, thawabu ya kusoma Qur-aan inamfikia Maiti?Je, hayo yalifanywa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au Makhalifa wake

 

3)    Waongofu au hata Swahaba zake watukufu?

 

4)   Madhara gani yanapatikana kwa kumsomea Qur-aan maiti.

 

5)   Na kama haifai basi ni jambo gani linalofaa kufanyiwa Maiti na litakalomsaidia? Haya ni maswali ambayo nimeyakusanya kwa ufupi kutoka kwa ndugu zetu waliouliza. Na nitajaribu kulijibu moja baada ya jingine kwa kadiri nitakavyowafikishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

a)  - Je kusoma Qur-aan Si 'Ibaadah Na jambo zuri? Kwa nini isifae kusoma Qur-aan kwenye Khitmah wakati Qur-aan ni du'aa?

 

Bila shaka taratibu zote za dini yetu zinatoka katika Qur-aan na Sunnah za kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na mipangilio yote ya ki'Ibaadah na Shari’ah kaishatufundisha yeye na katuwekea mipangilio safi isiyo na shaka wala isiyo na upungufu. Kwa hiyo lolote tutakalolifanya linapaswa liwe katika misingi hiyo miwili tuliyoitaja hapo juu; yaani kutoka kwenye Kitabu (Qur-aan) na Sunnah Sahihi za bwana wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Vilevile tunaweza kufuata na kuchukua kutoka kwa Makhalifa wake wanne Waongofu ambao ni Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu), 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu), 'Uthmaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) na 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwa ushahidi wa maneno yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema katika Hadiyth ndefu ambayo hapa mimi nitanukuu tu kipande hicho ninachokitolea ushahidi: "... Basi shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa wangu waongofu, kamataneni nazo kwa magego (shikamaneni nazo kwa nguvu zote)" [Abu Daawuud 4607, At-Tirmidhiy 2676] Nayo ni Hadiyth Nzuri Sahihi.

 

Kwa sababu hakuna popote pale kwa ushahidi sahihi panapothibitisha kusoma Qur-aan kwa Maiti, basi jambo hilo laingia katika Uzushi. Ni uzushi kwa sababu halikufundishwa wala halikutendwa si na Nabiy wala Makhalifa wake. Na katika Hadiyth hiyo hiyo hapo juu, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). anatutahadharisha sana na Uzushi au Bida'ah kwa kusema: " Na ole wenu na uzushi wa mambo (katika dini), hakika Kila bid'aa ni upotofu"

 

Pia usomaji huo unaosomwa katika Khitmah ni wa kelele na vurugu, kila mmoja husoma ki-aina yake na kwa kelele na wengi hawajui hata hukmu za tajwid. Na ingawa wanadai kuwa wanasoma Qur-aan kisha husoma na dua, Ukweli kusoma Qur-aan ni jambo zuri tena Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyopo kwenye [Al-Bukhaariy] na imesimuliwa na Abu Muwsa Al-Ash’ariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) anasema: “Mfano wa yule Muislam asomaye Qur-aan ni kama Utrujjah (tunda lenye harufu nzuri), harufu yake nzuri na ladha yake tamu. Na Muislam asiyesoma Qur-aan ni kama tende, haina harufu nzuri ingawa ina ladha nzuri.” [Al-Bukhaariy]

 

Hadiyth hii hata hivyo haikuja kwa kuwasomea Maiti Qur-aan bali ni kuisoma kila wakati na kuonyesha umuhimu wa kuisoma Qur-aan kwa waumini. Na Qur-aan hiyo hiyo ikisomwa nyakati nyingine huenda ikampatia msomaji dhambi badala ya thawabu! Mfano mtu akaisoma Qur-aan chooni, au akiisoma kwa kutaka kumlogea mtu n.k.

 

Na pia kuisoma kwa Maiti kwa sababu ni jambo la uzushi basi hupelekea katika madhambi na hata motoni kutokana na Hadiyth ya Nabiy katika riwaya nyingine aliposema:

 

"Kila bid'ah ni upotofu na kila upotofu ni motoni" (Allaah atuepushe na hilo)

 

Na Allaah Anasema:

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

Na inaposomwa Qur-aan, basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya (mzingatie) ili mpate kurehemewa. [A’raaf: 204]

 

Na kwenye Khitmah kila mmoja husoma kivyake na juzuu yake kwa sauti na hakuna mwenye kusikiliza.

 

Na anasema tena Allaah katika kuonyesha kuwa Yeye haihataji kuombwa kwa zogo na vurugu kwani Anajua akitakacho mja bila kupiga kelele na mayowe; Anasema:

 

وَاذْكُر رَّبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ

Na mdhukuru Rabb wako katika nafsi yako kwa unyenyekevu na kwa khofu na si kwa jahara katika kauli... [Al-A’raaf: 205]

 

Na wanasema kuwa wao wanamkumbuka Rabb wao na kumuomba, hata kama kuna makelele hakuna ubaya wowote; tunasema kuna ubaya kwani Allaah Amesema:

 

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

Muombeni Rabb wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye Hapendi wenye kupindukia mipaka[Al-A’raaf: 55]

 

b)    -  Je, Thawabu Ya Kusoma Qur-aan Humfikia Maiti?

 

Naye Imaam An-Nawawiy katika kufafanua kitabu cha Hadiyth cha Imaam Muslim, kwenye Hadiyth hiyo akasema: “Ama kusoma Qur-aan na kukusudia thawabu za kisomo chake kimwendee maiti, na kuswali ili thawabu zake zimfikie na mfano wa haya, amesema Imam Ash-Shaafi’iy na Jamhuur ya Wanachuoni (yaani Wanachuoni wengi) kwamba haya hayamfikii maiti”

 

Imam Ash-Shaafi’y alipoulizwa kuhusu hilo akajibu kuwa thawabu ya kisomo haimfikii maiti na akatolea dalili hoja yake kwa Aayah isemayo: 

وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ

Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi. [An-Najm: 39]

 

Na pia akatoa ushahidi wa Hadiyth:

 

“Anapokufa mwanaadam hukatika amali zake ila kwa mambo matatu...” Taz. kitabu chake maarufu Al-Umm Juzuu ya 4, uk. 46 

 

Pia katika kitabu maarufu cha madhehebu ya Ki-Shaafi’iy kiitwacho Al-Minhaaj, katika ufafanuzi uliofanywa na Ibnu Nahwy ni kwamba: “Hazimfikii maiti katika madhehebu yetu thawabu za kisomo katika kauli mashuhuri.”

 

Aliulizwa Shaykh Al-‘Izz bin 'Abdis-Salaam, Mwanachuoni mkubwa wa Misr katika zama zake kama thawabu za kisomo kinachotolewa hidaya kwa Maiti (yaani kwa Niyah thawabu zake zimfkie Maiti) kwamba thawabu zake zitamfikia au hapana? Akajibu:

 

“Thawabu za kisomo huzipata msomaji wala hazifiki kwa mwengine” Taz. kitabu cha Hukmu Qiraat Lil Amwaat uk. 24

 

Katika kitabu cha As-Sunanu wal Mubtada’aat uk. 216 kuhusu kumsomea Maiti Qur-aan, anasema mwandishi.

 

"Na kisomo cha Khitmah ambazo wanazozifanyia watu waliokufa na kukusanyika kwenye Khitmah hizo kwa kisomo, na kutawanyiana Juzuu... kutoka katika Msahafu kisha wanaanza kisomo na kumaliza kwa pamoja kwa kitambo kidogo tu kisha hupeleka hidaya thawabu walizozisoma kwa Maiti, ni Bid'ah yenye upotofu, mfanyaji wake yuko kwenye upeo wa ujinga."

 

Naye Mwanachuoni mkubwa maarufu wa Tafsiyr ya Qur-aan, Imaam Ibn Kathiyr katika Tafsiri ya Suwrah Najm Aayah ya 39 ameeleza kutokufaa kusoma Qur-aan na kufika thawabu zake kwa maiti.

 

Ni wanachuoni wengi maarufu wa kale wa Ki-Shaafi’iy waliopinga jambo hilo na sitoweza kuwataja wote waliyoyasema bali nitawataja baadhi yao tu kama wanafunzi wakubwa wa Imaam Ash-Shaafi’iy, Al-Muzaniy, Abu Ishaaq Ash-Shiraziy na wengine wengi. Ukiachilia mbali msururu wa mamia ya Wanachuoni wa madhehebu nyingine na wale ambao hawajifungamanishi na madhehebu yoyote.

  

c)  - Je, Hayo Yalifanywa Na Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Au Makhalifa Wake Waongofu Au Hata Swahaba Zake Watukufu?

 

Hakuna ushahidi wowote wala Hadiyth yoyote sahihi au hata dhaifu inayoonyesha kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kusoma Khitmah au kuwaambia watu wakusanyane na wamsomee maiti wao Qur-aan. Zipo Hadiyth dhaifu na za kutungwa (mawdhuw') zinasema kuwa maiti asomewe Suwrah Yaasiyn au Suwrah Faatihah au Ikhlaasw (Qul Huwa Allaahu Ahad) mara kumi na moja makaburini! Kama nilivyosema kuwa zote hizo ima ni dhaifu au za uongo (mawdhuw') na haziwezi kuwa ni Hoja au kujengea Shariy’ah au mpangilio na taratibu katika jambo lolote la dini!

 

Hivyo basi, hakuna ushahidi popote pale kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala Makhalifa wake waongofu au hata Maswahaba kwamba walifanya Khitmah.

 

Kuna baadhi ya watu wa Khitmah wanaodai kuwa wakati ule Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akifiwa na watu wake au marafiki zake na Swahaba kwa ujumla; kuwa Qur-aan ilikuwa haijashuka yote na hivyo asingeweza kufanya Khitmah. Dai la namna hii ni dai potofu kwa sababu nyingi, baadhi yake ni kuwa; huko ni kumfanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa hakuwa na maarifa kamili ya dini hii, na kwamba kuna mambo muhimu ya dini yetu aliyoyaacha na hakutufikishia (Allaah Atuepushe na dhana kama hizo).

 

Jibu lingine ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifiwa na binti yake Ummu Kulthuum katika mwaka wa sita, na hapo Qur-aan ilikuwa imeshuka taqriban yote; sasa kwanini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asimsomee huyo mwanawe mtukufu kama jambo hilo lina manufaa kwa maiti?

 

Na hata alipokufa yeye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) vipenzi vyake kama Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu), ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hawakumsomea pamoja na kuwa Qur-aan ilikuwa ishakamilika na wao walikuwa na uchungu naye kuliko mimi au sisi tunaosoma Khitmah kwa maiti wetu.

  

d)    - Madhara Gani Yanapatikana Kwa Kumsomea Qur-aan Maiti?

 

Madhara makubwa sana yanayopatikana katika jambo hili ni Uzushi. Kuzusha jambo katika dini yetu hii jambo ambalo halikuwepo na halijafundishwa wala kufanywa wala kuridhiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Nabiy amekemea sana kwenye Hadiyth nyingi mno kuhusu ubaya wa Uzushi na Bid'ah.

 

Anasema katika Hadiyth aliyopokea mama wa Waumini, ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha):

 

“Mwenye kuanzisha jambo katika dini yetu hii, ambalo halimo, hurejeshewa nalo (halikubaliki mbele ya Allaah)” [Al-Bukhaariy, 2697]

 

Nyingine:

 

“Mwenye kufanya jambo ambalo halimo katika jambo (Dini, Shari’ah) letu, basi huwa linamrejelea mwenyewe” [Muslim, 1718]

 

Nyingine tushaitaja huko mwanzo nayo:

 

“Nawausieni Uchaji Allaah na usikivu na utiifu hata kama akiwa kiongozi wenu ni mtumwa (katika riwaya nyingine mtumwa mhabashi), na hakika atakayeishi baada yangu ataona khitilafu (tofauti) nyingi, basi (mtakapoona hali hiyo ya uzushi na kuchafuliwa katika Dini) shikamaneni na Sunnah (mwenendo) wangu, na Sunnah (mwenendo) wa Makhalifa wangu waongofu, na mzibane kwa magego (mzikamate kisawasawa). Na tahadharini na uzushi, hakika kila uzushi ni bid'ah na kila bid'ah ni upotevu” [Abu Daawuud 4607 na At-Tirmidhiy 2676] katika riwaya nyingine 'kila upotevu ni kwenye Moto (wa Jahannam)'

 

Nyingine:

 

“...Uzuri wa maongezi ni maongezi ya Kitabu cha Allaah, Na ubora wa uongofu ni uongofu ulioletwa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na uovu wa mambo ni uzushi, na kila uzushi ni upotofu” [Muslim, 425]

 

Na Hadiyth ziko nyingi sana za kukemea na kuonyesha mafikio mabaya kabisa ya mtu anayezusha (Mzushi) mambo mbalimbali katika dini.

 

Na pia Hadiyth nyingine na maneno ya Wanachuoni yanatuonyesha ni jinsi gani kuna umuhimu na ubora wa kukamatana na kushikamanana na Sunnah za Nabiy wetu mpenzi (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwa kila tunavyokamata Sunnah au kuzihuisha (kuzifufua) ndipo ujira wetu na kheri zinavyoongezeka. Na kukamatana na Bid'ah kunakimbiza kheri baraka na kueneza ufisadi na maasi katika jamii. Na ni bora kutosheka na Sunnah chache kuliko kukamatana na bid'ah nyingi.

 Mwisho tuangalie kipengele cha tano chenye kuuliza:

 

e)    - Na Kama Haifai Basi Ni Jambo Gani Linalofaa Kufanyiwa Maiti Na Litakalomsaidia?

 

Hadiyth maarufu sana inayojulisha kuwa mwanaadam akifa hukatika matendo yake yote ila mambo matatu tu ndiyo yatakayomsaidia wakati yeye hayupo tena duniani; nayo ni sadaka iendeleayo (itumikayo), elimu inufaishayo watu na mwana mwema anayemwombea. Na haya ndiyo mambo ambayo tushaelezwa na Mtukufu wa daraja na Mpenzi wetu mkubwa aliyetupendea kila zuri na la kheri, sasa kwa nini tujizonge na kujitaabisha kwa mengine ya ziada yasiyo na faida wala manufaa zaidi ya kutuchosha na kutugharimu na baya zaidi kututia madhambini.

 

Imaam An-Nawawiy anasema katika kitabu chake cha Al-Adhkaar uk. 150 hivi:

 

“Wamekubaliana Wanachuoni kwamba du’aa za kumwombea maiti zinawanufaisha na zinafika thawabu za du’aa hiyo. Na wametoa hoja na dalili ya kauli yake Allaah aliposema:

 

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ

Na wale waliokuja baada yao wanasema: Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan.. [Al-Hashr: 10] 

 

“Na nyinginezo miongoni mwa Aayah mashuhuri zenye maana kama hiyo; na katika Hadiyth nyingi zilizo mashuhuri kama vile maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Ee Rabb wangu! Wasamehe watu wa Baqi’i Alghardaq”

na pia aliposema:

 

“Ee Rabb wangu! Wasamehe walio hai wetu na waliokufa wetu” na Hadiyth nyinginezo"

 

Mwisho wa maneno ya Imaam An-Nawawiy.

 

Pia ‘Ulamaa wanaonelea kuwa miongoni mwa sadaka ni kumfanyia maiti ‘Umrah au Hajj ikiwa alikuwa hajafanya kwa ushahidi huu:

 

“Mwanamke wa kabila la Juhaynah alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Mama yangu alikuwa na nadhiri ya kufanya Haji je, naweza kumlipia (kumhijia)? Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Akamjibu: “Mhijie. Je, mama yako angekuwa na deni usingemlipia? Basi, deni la Rabb wako ni bora zaidi kulilipa” [Al-Bukhaariy]

 

Na vilevile wanaonelea kuwa mtu anaweza kumfungia maiti yake Swawm ya nadhiri au aliyokuwa anadaiwa hajailipa kwa ushahidi huu:

 

“Alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Ee Rasuli wa Allaah! Mama yangu amefariki na alipaswa kufunga Swawm ya mwezi mmoja (aliyokuwa akidaiwa) Je, naweza kumfungia? Nabiy akajibu kwa kuitikia kisha akamwambia: “Deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa” [Al-Bukhaariy]

 

Wengine wanaonelea kuwa yafaa hata kumlipia zile Swawm za deni kama mwanamke aliyekuwa katika siku zake. Lakini si Swawm za Sunnah au zile mtu alizoziacha kwa makusudi.

 

Haya ni mambo ambayo ni bora kuyafanya na yana ushahidi sahihi na ndio bora Waislam wakayafanyia kazi zaidi kwani ndio yenye manufaa kwa wenzetu waliotangulia.

 

Namalizia hapa kwa kuwanasihi ndugu zangu turejee katika njia sahihi na mafundisho sahihi ya mtukufu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na tuyaache yenye mashaka na yenye kutusababishia madhara katika Dini yetu.

 

Mwisho namwomba Allaah Atuongoze wote sisi katika njia iliyonyooka na atusamehe tuliyoyafanya bila elimu au kwa kurithi wazee na Masheikh wetu bila ya dalili, na Atujaalie ni wenye kusikiza maneno na kufuata yaliyo mema.

 

Wa Allaahu A’lam

 

Share