Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

  

 

Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Ndugu Waislamu, tunachukua fursa hii ya kunasihi  kwa kufuata amri ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na Hadiyth: 

 

  عَنْ تَمِيمٍ الدَّارِيِّ أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ :((الدِّينُ النَّصِيحَةُ قُلْنَا لِمَنْ قَالَ لِلَّهِ وَلِكِتَابِهِ وَلِرَسُولِهِ وَلِأَئِمَّةِ الْمُسْلِمِينَ وَعَامَّتِهِمْ)) مسلم

Kutoka kwa Tamiym Ad-Daariyyi kwamba Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Dini ni Nasiha)). Tukasema kwa nani? Akasema: kwa Allaah na Kitabu Chake na Rasuli Wake, na kwa Viongozi wa Kiislam na watu wa kawaida)) [Muslim]

 

Waislamu tunatakiwa daima tuwe wenye kupeana nasiha za kuamrishana mema na kukatazana maovu. Kunasihiana katika jambo kama hili la kusambaza Hadiyth dhaifu ni jambo muhimu zaidi kwani kuna hatari kubwa ndani yake kama tuonavyo maonyo yaliyomo katika Qur-aan na Sunnah. Imewajibika kutoa nasaha hizi kutokana na uzushi wa makala, Hadiyth zisizo Swahiyh, au ujumbe mbalimbali unaoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

 

Mfano wa ambayo yanazushwa pamoja na dalili za makatazo yake:  

 

 

Shaykh Swaalih Al-Fawzaan - Jumu'ah Mubaarakah Haijathibiti

 

 

Shaykh Fawzaan: Kuomba: Ee Allaah! Tubarikie Rajab Na Sha´baan Na Tufikishe Ramadhwaan Ni Swahiyh?

 

 

Uzushi Wa Kuomba Maghfirah Katika Mwezi Wa Rajab

 

 

Hakuna ‘Ibaadah Maalumu Wala Swawm Wala Du’aa Makhsusi Kwa Ajili Ya Mwezi Wa Rajab

 

 

Mwezi Wa Rajab: Fadhila Zake Na Yaliyozuliwa Ndani Yake

 

 

Kufunga Na Kusherehekea Siku Inayosemekana Ni Ya Israa na Mi'iraaj

 

Fatwa: Du’aa Ya Mwezi Wa Rajab Sha’baan na Ramadhwaan Haikuthibiti

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Du’aa Makhsusi Ya Mwezi Wa Rajab Sha’baan na Ramadhwaan Imethibiti?

 

Uzushi Wa Mashia Wa Swalah Ya Usiku Wa Mwanzo Wa Sha'baan

 

 

Tanabahi Kuhusu Bid'ah (Uzushi) Ya Nusu Ya Sha’baan; Kufunga Swawm, Kumdhukuru Allaah Na Kuomba Du’aa

 

 

Sha'baan - Fadhila Zake Na Uzushi Wa Niswfu Sha'abaan

 

 

Kufunga Na Kukutanika Usiku Wa Niswf Sha’baan Na Kufanya Kisomo Inafaa?

 

 

Uzushi Niswfu Sha'baan Na Kuhusu Qismatu Rizq (Mgawanyo Wa Rizki)

 

 

Fatwa: Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Du’aa "Allaahumma Balighnaa Ramadhwan" Haikuthibiti

 

Fatwa: Du’aa "Allaahumma Balighnaa Ramadhwan", Haikuthibiti

 

Swalah Za Siku Kumi La Mwisho Wa Ramadhwaan Sahihi Au Uzushi?

 

 

Uzushi Wa Adhkaar Baada Ya Kila Rakaa Za Swalaah Ya Taraawiyh

 

 

Uzushi Wa Swalaah Ya Ijumaa Ya Mwisho Katika Ramadhwaan Kukidhia Swalaah Na Kuwa Inafuta Madhambi

 

 

Uzushi Wa Unoadaiwa Ni Fadhila Za Siku Kumi Za Dhul-Hijjah

 

 

Uzushi Unaodaiwa Kuhusu Mambo Yaliyotokea Siku Ya 'Aashuraa Tarehe 10

 

 

Uzushi Kuhusu Swalah Maaulum Ya Jumatano Ya Mwisho Mfungo Tano (Swafar)

 

 

Du'aa Za Kanzul-Arsh Na Du'aa Za Masiku Ya Wiki Zimethibiti?

 

 

Du’aa Ya Kanzul-'Arsh (Ganjul-'Arsh) Ni Uzushi Wa Mashia Na Masufi

 

 

Kitabu Cha Du'aa Kiitwacho 'Ad-Du'aa Al-Mustajaab' Kimejaa Uzushi Mkubwa

 

 

Uzushi Wa Du’aa Ya Mara Moja Katika Umri (Maisha)

 

 

Du’aa Ya ‘Al-Jawshan Al-Kabiyr’ (Diraya Kubwa) الجوشن الكبير

 

 

Uzushi Wa Kitabu Cha Aayatul-Kifaayaah

 

 

Hadiyth Ya "Ewe 'Aliy Fanya Mambo Matano Kabla Ya Kulala" Ni Sahihi?

 

 

Swalah Za Uzushi KuhusuTahajjud Na Usiku Wa Ijumaa

 

 

Uzushi Wa Kisa Cha 'Alqamah

 

 

Mengineyo Yanayozushwa ni:

 

-Barua kutoka kwa Shaykh Ahmad wa Madiynah ameota kuhusu Qiyaamah.

 

-Malaika mkubwa na mdogo.

 

-Acha kufanya kila jambo unaposikia Adhana.

 

-Fadhila za Majina 99  ya Allah.

 

-Malaika watano wakati mtu anakufa.

 

-Adhabu kumi na tano za mwenye kuacha Swalaah.

 

 

Kwa hiyo Muislamu anapaswa pindi inapomfikia khabari yoyote inayohusiana na ‘ibaadah zetu au Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi huwa ni waajib kwake  ahakikishe usahihi wa kauli au Hadiyth hiyo. Ikiwa imetambulika kuwa ni Swahiyh baada ya utafiti na kuuliza wenye elimu, hapo unaweza kuwatumia wenzako ili wafaidike nawe upate fadhila zake.  Lakini pindi ikitambulikana kuwa ni dhaifu, uzush, basi haikupasi kusambaza bali anapswa aifute haraka, kwa sababu pindi akisambaza itakuwa ni kubeba dhambi na dhambi za wataokafanyia kazi mafunzo hayo ya uzushi.

 

Dalili zifuatazo zinataja manufaa na madhara ya kusambaza ‘elimu ikiwa ni Swahiyh au uzushi.

 

 

Hadiyth ya kwanza:

 

عن أبي مسعود الأنصاري رضي الله عنه يقول النبي صلى الله عليه وسلم : (( مَنْ دَلَّ عَلَى خَيْرٍ فَلَهُ مِثْلُ أَجْرِ فَاعِلِهِ)) مسلم في صحيحه .

((Mwenye kuongoza katika kheri atapata thawabu kama za mwenye kufanya)) [Muslim katika Swahiyh yake]

 

 

Hadiyth ya pili:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : ((مَنْ دَعَا إِلَى هُدًى كَانَ لَهُ مِنْ الْأَجْرِ مِثْلُ أُجُورِ مَنْ تَبِعَهُ لَا يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْئًا، وَمَنْ دَعَا إِلَى ضَلَالَةٍ كَانَ عَلَيْهِ مِنْ الْإِثْمِ مِثْلُ آثَامِ مَنْ تَبِعَهُ لَا يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ آثَامِهِمْ شَيْئًا))   رواه مسلم  

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema ((Atakayelingania kwenye uongofu atapata thawabu (ujira) wa yule atakayemfuata bila ya kupungukiwa chochote katika thawabu zao. Na atakayeelekeza katika upotofu atapata dhambi mfano wa dhambi za yule atakayefuata bila ya kupungukiwa chochote katika dhambi zao)) [Muslim]

 

Hadiyth ya tatu:

 

 

عَنْ جَرِيرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ رضي الله عنه عن النبيّ صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ سَنَّ فِي الإِسْلامِ سُنَّةً حَسَنَةً فَلَهُ أَجْرُهَا وَأَجْرُ مَنْ عَمِلَ بِهَا بَعْدَهُ مِنْ غَيْرِ أَنْ يَنْقُصَ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْءٌ وَمَنْ سَنَّ فِي الإِسْلامِ سُنَّةً سَيِّئَةً كَانَ عَلَيْهِ وِزْرُهَا وَوِزْرُ مَنْ عَمِلَ بِهَا مِنْ بَعْدِهِ مِنْ غَيْرِ أَنْ يَنْقُصَ مِنْ أَوْزَارِهِمْ شَيْءٌ ))  مسلم  

 

"Atakayeanzisha mwenendo mwema " سُنَّةً حَسَنَةً katika Uislamu atapata ujira wake na ujira wa atakayetenda wema huo bila ya kupungua kitu katika ujira wa waliotenda, na atakayeanzisha mwenenedo mbaya سُنَّةً سَيِّئَةً atapata madhambi yake na madhambi ya atakayetenda madhambi hayo bila ya kupungua kitu katika madhambi yao " [Muslim] 

 

 

 

Kusambaza Hadiyth bila ya kuhakisha kama ni Swahiyh kutasababisha madhara yafuatayo

 

 

Kwanza: Kujiandalia Makazi ya Moto:

 

 ((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه

((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni))  [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

Na kama tunavyoona kwamba hatari yake ni kujitayarishia makazi motoni (tunamuomba Allaah Atuepushe na hilo). Hivyo pia tutakuwa tumewaingiza na wenzetu ambao nao wataendelea kuzisambaza hizo Hadiyth na itaendelea hivyo hivyo kuwaingiza ndugu zetu wengi katika hatari kama hii. Na hatari zaidi ni kwamba kila watu wanapozidi kuzisambaza, basi dhambi huzidi kuongezeka kwa waliotuma wote nyuma yao na haswa zaidi kwa aliyeanzisha, (maana kwamba, wingi wa dhambi unazidi kuongezeka na wa mwanzo kabisa ndiye mwenye kubeba dhambi za watu wote)  

 

 

Pili:  Kupoteza Wakati Kwa Ajili Ya ‘Amali Zisizokubaliwa

 

 

Hadiyth hizo zitazidi kusambaa na wengi wasioweza kupambanua baina ya Hadiyth Swahiyh na Hadiyth dhaifu watakuwa wanaona ni sawa kwao na watakuwa wanapoteza wakati wao kutekeleza ‘ibaadah zinazotajwa fadhila zake katika Hadiyth hizo dhaifu na wasipate thawabu yoyote, wakati wangeliweza kuutumia wakati wao na nguvu zao kwa ‘ibaadah zilizokuwa na uhakika zilizothibiti kwa ushahidi sahihi na wakapata ujira.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾

Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya   chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika. [Al-Furqaan: 23]

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anasema:

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa  na mafunzo ya dini yetu basi kitarudishwa.)) [Al Bukhariy] 

 

Jambo Muhimu La Kuzingatia:

 

‘Ibaadah zetu zote ikiwa ni kwa vitendo au kauli basi ni lazima zutimize sharti mbili muhimu kabisa  nazo ni:

 

i-Ikhlaas – Iwe kwa kutaka Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  na sio yenye Riyaa (kujionyesha) au sio yenye kutendeka kwa ajili ya       maslahi ya kidunia.

 

ii-Iwe inatokana kwa mujibu wa mafunzo ya Qur-aan na Sunnah.  

 

 

Tatu:  Kupoteza Mafunzo Sahihi Na Badala Yake Ni Kuenezea Mafunzo Ya Uzushi

 

Dhara nyengine ya  jambo hili ni kwamba, kila zinapoendelea kusambaa Hadiyth hizo dhaifu, ndipo Hadiyth sahihi nazo zinaachwa kutumika na kujulikana, na mwishowe ni kuenea mafunzo yasiyo sahihi ya uzushi na kupotea yale yaliyo sahihi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ameonya:    

 

(( وأياكم ومحدثات الأمور فإن كل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة))

((Jihadharini na mambo ya uzushi kwani kila uzushi ni Bid'ah na kila Bid'ah ni upotofu))

 

Nne:   Ukosefu Wa Mapenzi Ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

  

Tutambue kuwa kuhakikisha kwamba Hadiyth Sahihi za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  zinabakishwa na Hadiyth dhaifu zinafutwa ni ishara ya mapenzi makubwa kwa ambaye anayempenda kwa dhati Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwa sababu hakuna mtu apendaye kumzulia mpenzi wake maneno asiyoyasema. Na kinyume chake ni ukosefu wa mapenzi ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Nani basi katika sisi mwenye kumpenda kwa dhati Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?   Je, ni yule mwenye kumsambazia tu uzushi bila ya kujali au yule mwenye kujali na khofu ya kumsambazia uzushi?  

 

 

Tanbihi:

 

Ukipokea jambo lolote lenye mashaka na utata kuhusiana na Dini, tafadhali tuma kupitia  maswali@alhidaaya.com lifanyiwe utafiti kabla ya kuwatumia wengine na kuenezwa, na tutajaribu kujibu haraka In Shaa Allaah. 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atujaalie nuru ya elimu Yake na Atuonyeshe yaliyo ya haki tuyafuate na yaliyo ya batili tuepukane nayo.

 

 

 

 

 

 

Share