Wanawake Wananikimbia - Je, Jini Linaweza kumuoa Binaadamu?

 

 

Wanawake Wananikimbia - Je, Jini  Linaweza kumuoa Binaadamu?  

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Hilo Ndio Swali Langu, Jibu Lisiwe Kumuacha Naamini Kila Kitu Kina Jibu Lake Kwa Mungu. Na Je Jini Linaweza Kumuowa Binaadamu Au Kuwa Na Wivu.

 

Tatizo linalo ni kuwa kila nitapokuwa na mwanamke muda si mrefu mwanake atanikimbia na umefikia umri wa kuoa katika kufuatilia kutaka kujua tatizo nini lakini wataamu wa mambo wanasema kuwa ninajini la kike ndilo linanifukuzia wanawake sasa mimi nataka ufumbuzi wa swala hili,alhidaya mimi si mgeni kwenu, nawatakia kila la kheri kama kunauwezekano nipate number yenu ya simu nitawapigia

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo. Nasi hapa tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe dawa na Akuondolee ugonjwa ulionao. Hata hivyo, tunasikitika sana kusikia wewe unataka dawa na huku unamuasi Allaah katika maamrisho yake.

 

Itakuwaje wewe kama Muislamu uwe unacheza na wanawake wa watu? Je, utalikubalia hilo kwa dada yako, au mamako, au mkeo au shangazi yako au jamaa yako yeyote? Hilo huwezi kukubali kabisa. Vipi basi unakuwa ni mwenye kuwa na mwanamke mmoja na mwingine kinyume cha sheria? Uislamu umekataza mas-ala ya mwanaume na mwanamke kuwa na urafiki. Ikiwa kweli uko tayari kuoa unatakiwa uwashirikishe jamaa zako hasa wale wa kike ili wakusaidie katika kupata mchumba bila ya kufanya urafiki naye. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

 

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32].

 

Hakika ni kuwa jini hawezi kuolewa au kuoa binadamu lakini huweza kumvaa mwanadamu na akawa anajamiiana naye. Ikiwa mwanamme amevaliwa na jini la kike basi humsababishia huyo mume asiwe ni mwenye kupata mke. Jini ni kama mwanadamu ana wivu, na mume anapooa basi huyo jini hujawa na wivu na hufanya kila njia ili mume na mke wakosane.

 

Hili si suala gumu la kutatuliwa katika njia ya kisheria. Hakika ni kuwa zipo njia nyingine huzidi kuleta taabu na zinamtia mwenye kufanya katika ushirikina. Linalotakiwa ni wewe kwenda kwa msomi mcha wa Allaah akusomee Qur-aan kwa Aayah za kumtoa huyo jini wa kike na hapo hutakuwa na tatizo. Baada ya kutolewa huyo jini inatakiwa ujikinge na Ruqyah (zinguo) la kisheria wewe mwenyewe ili asirudi tena. Mbali na kujiwekea muda wa kusoma sehemu ya Qur-aan kila siku pia ni vyema uwe unasoma zile Aayah za kukukinga na shetani pamoja na du’aa alizotufundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zake. Na kijitabu kizuri katika mas-ala haya ni Hiswnul Muslim.

 

Lakini nasaha yetu kwako ni kuwa bila kuacha dhambi hilo la kufuata wanawake basi na jini hilo halitakuwa ni lenye kutoka. Kuwa katika kumtii Allaah na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na utekeleze ‘Ibaadah inavyotakiwa na uache aina yoyote ya uasherati na maasi.

 

Tunakuombea mafanikio mema In shaa Allaah. 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share