Hadiyth Ya Al-Jassaasah

 

Hadiyth Ya Al-Jassaasah

 

Imetarjumiwa Na: Muhammad Faraj Saalim As-Sa'iy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Utafiti mwingi uliofanywa na wazungu wenye kufuatilia mambo ya ulimwengu wa Mashariki (Orientalists) juu ya dini ya Kiislamu na juu ya Nabiy wa Waislamu katika nadharia zao wanaitakidi kuwa mengi kati ya yaliyomo ndani ya mafundisho ya dini ni miongoni mwa itikadi zilizokuwepo wakati ule alioishi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kwa maana nyingine ni kuwa kwa vile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliishi karibu na Mayahudi na Manasara, akaingiliana nao, na wakaingia baadhi yao katika dini ya Kiislamu kumesaidia sana katika kuingiza itikadi zao na kuzifanya kuwa sehemu ya dini hii mpya.

 

 

Kusudi la nadharia yao hii ni kuingiza shaka katika utukufu wa ujumbe huu wa mwisho kwa njia ya kuwaambia watu kuwa; Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuja na kipya katika mambo ya Ghaibu na mambo ya Imani, na kwamba yote anayofundisha ni katika itikadi na ibada zilizokuwepo tokea mwanzo.

Utayaona hayo kwa uwazi katika kamusi mbalimbali za maarifa na vitabu vilivyowekwa kwa ajili ya kuwafundisha watu juu ya dini ya Kiislamu, elimu yake na viongozi wake likiwemo kamusi maarufu 'Daairat al-Maarif al-Islamiyah', walioshirikiana kuliandika wengi katika watu maarufu wenye kushughulikia mambo ya ulimwengu wa Mashariki.

 

 

Tutakuta kwa mfano waliyoandika kuhusu 'Tamiym ad-Daariy', ambaye yumo katika maudhui yetu haya.

 

 

Anasema mtaalamu wa mambo ya ulimwengu wa Mashariki kutoka Italia Levy Dalavida:

"Na Tamiym alikuwa mfuasi wa dini ya Kinasara kama walivyokuwa wengi kati ya waarabu wa Syria, akafanikiwa kumfundisha Nabiy juu ya ibada nyingi alizojifunza katika dini ya kinasara…. Na inasemekana kuwa Tamiym ndiye wa mwanzo kumhadithia Nabiy visa mbalimbali vya dini, Nabiy akavisadiki na kuwahadithia watu."

(Mwisho wa maneno ya Levy)

 

 

Wakaja wapungufu wa elimu waliofuata maneno haya ya wataalamu hawa wa ulimwengu wa Mashariki na kuyakubali maneno yao kama kwamba ni ukweli usiopingika. Wakazitilia shaka Hadiyth Swahiyh zilizoandikwa na kuthibitishwa katika vitabu sahihi kupita vyote, na zilizopokelewa kupitia masdari sahihi, kwa hoja kuwa eti watu wa kitabu 'Ahlul-Kitaab' wameingiza maneno yao ndani yake.

 

 

Sisi hatukanushi kuwa zipo Hadiyth nyingi za watu wa kitabu, pamoja na tafsiri zao zilizojipenyeza ndani ya vitabu vyetu, na hizi ni habari na visa maarufu ziliokwishatajwa na ‘Ulamaa na kuzibainisha kwa watu. Lakini kutumia kisingizio hiki kwa ajili ya kuzikataa Hadiyth Swahiyh zilizothibiti, au kuzitumia kwa ajili ya kuwatuhumu Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum), walioisimamia na kuisimamisha dini hii, ni jambo lisilokubaliwa na Muislamu yeyote.

 

 

Mjadala uliozushwa zaidi kuhusu Riwaayah za Tamiym ni juu ya kisa cha Al-Jassasaah kilichomo ndani ya [Swahiyh Muslim]

 

 

Kisa hiki kilisimuliwa na Faatwimah bint Qays (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa akiwahadithia watu juu ya kisa cha Ad-Dajjaal kama alivyokisikia kutoka kwa Tamiym aliyekuwa katika dini ya Kinasara kisha akasilimu. Alimuhadithia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Hadiyth iliyokubaliana na aliyokuwa akiwahadithia Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) juu ya Ad-Dajjaal na wafuasi wake.

 

 

Na Kisa Chenyewe Ni Kama Ifuatavyo:

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa juu ya Minbari huku akicheka akasema: "Kila mtu aushikilie vizuri mswala wake. Kisha akasema: "Mnajua kwa nini nimekukusanyeni (nimekuiteni)?" Wakasema: "Allaah na Nabiy wake ndio wanaojua." Akasema: "Mimi Wa-Allaahi sikukuiteni kwa ajili ya kukupendezesheni wala kukutisheni, lakini nimekuiteni kwa sababu Tamiym Ad-Daariy aliyekuwa akifuata dini ya kinasara amekuja kufungamana na mimi na kusilimu. Na amenihadithia Hadiyth inayokubaliana na niliyokuwa nikikuhadithieni juu ya Masiyh Ad-Dajjaal. Amenihadithia kuwa:

 

"Tulipanda merikebu baharini pamoja na wanaume thelathini wa kabila la Lakhm na Judham, na mawimbi yakatuchezea baharini mwezi mzima, mpaka tulipokifikia kisiwa wakati wa magharibi na watu wakakaa ukingoni mwa merikebu (au juu ya ngalawa ya kushushia watu). Wakaingia kisiwani wakamkuta mnyama mwenye nywele nyingi sana, kwa wingi wa nywele hajulikani wapi mbele wapi nyuma.

Wakasema: "Ole wako! Nani wewe?"

Akasema: "Mimi ndiye Jassaasah."

Wakasema: "Nini Jassaasah?"

 

Akasema: "Enyi watu, nendeni kwa huyu mtu kijijini hakika yeye atakuwa na hamu kubwa ya kujua habari zenu." Akasema: "Alipotajia jina lake tukahofia asije kuwa shetani." Akasema: "Tukaondoka haraka mpaka tulipowasili kijijini, na hapo tukamuona mtu mkubwa hatukupata kuona mfano wake kimaumbile. Mikono yake imefungwa shingoni pake na amefungwa kwa vyuma kuanzia magotini mpaka visigino vya miguu yake."

 

Tukamuambia: "Ole wako, nani wewe?"

Akasema: "Mumekwishazijua habari zangu, nihadithieni juu yenu. Ni nani nyinyi?"

 

Wakasema: "Sisi ni watu katika waarabu, tulisafiri kwa merikebu na ikasadifu bahari kuchafuka. Mawimbi yakatucheza muda wa mwezi kisha tukateremka katika kisiwa chako hiki. Tukakaa ukingoni mwa merikebu na tulipoingia kisiwani tukakutana na mnyama mwingi wa nywele hajulikani wapi mbele wapi nyuma kwa wingi wa nywele tukamuuliza, 'Ole wako, Nani wewe?' Akasema: 'Mimi ni Jassaasah', tukamuuliza: 'Nini Jassaasah?' Akatuambia nendeni kwa mtu huyu kijijini atakuwa na hamu ya kujua habari zenu. Ndipo tulipokujia wewe haraka na tulimuogopa, tukidhania kuwa anaweza kuwa shaytwaan.'

 

Akasema: Nipeni habari za mitende ya Biysan.'

Tukamuuliza: 'Nini katika habari zake unataka kujua?'

Akasema: 'Nataka kujua juu ya tende zake. Zishamea? Tukamuambia: 'Ndio'.

Akasema: "Hivi karibuni zitaacha kumea."

Akasema: "Nipeni habari za bahari ya At-Twabariyah."

Tukamuuliza: "Nini katika habari zake unataka kujua?"

Akasema: "Yamo maji ndani yake?"

Wakasema: "Maji mengi sana."

Akasema: "Hakika hivi karibuni maji yake yatatoweka."

Akasema: "Nipeni habari za ‘Ayn Zaatar."

Wakasema: "Nini katika habari zake unataka kujua?'

Akasema: "Katika chemchem yake yamo maji?

Wakasema: "Ndiyo, maji mengi sana, na watu wake wanayatumia kwa kilimo chao."

Akasema: "Nipeni habari za Nabiy wa wasiojua kusoma wala kuandika amefanya nini?"

Wakasema: "Ameondoka Makkah na kuhamia Yathrib (Madiynah)."

Akasema: "Wamempiga vita waarabu?"

Tukasema: "Ndiyo.'

Akasema: "Na yeye amewafanya nini.?

Tukamjulisha kuwa amehamia kwa waarabu wengine wenye kumuunga mkono na kumtii."

Akawaambia: "Yashatokea hayo?"

Tukasema: "Ndiyo."

 

Akasema: ‘Ama ni bora kwao kumtii. Na mimi nitakupeni khabari zangu. Mimi ndiye Al-Masiyh, na hivi karibuni nitapewa idhini ya kutoka na nitatoka na kutembea juu ya ardhi, na wala sitoacha kijiji ila lazima nikipitie katika muda wa siku arubaini isipokuwa Makkah na Twiybah (Madiynah), miji hii ni haramu kwangu kuingia ndani yake. Kila ninapotaka kuingia katika mojawapo ya miji hiyo, ananikabili Malaika aliyeshika mkononi mwake upanga ulionolewa akinizuia. Hakika katika kila pembe yupo Malaika mwenye kuilinda miji hiyo.

 

Akasema Faatwimah bint Qays (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ‘Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema huku akichocha gongo lake katika Minbari: "Hii ndiyo Twiybah hii ndiyo Twiybah hii ndiyo Twiybah (akimaanisha Madinah). Si nilikuhadithieni haya?" Watu wakasema: "Ndiyo."

 

Akasema: "Kwa hakika imenifurahisha Hadiyth ya Tamiym kwa kuwa inakubaliana na yale niliyokuhadithieni juu ya Madiynah na Makkah. Hakika atatokea katika bahari ya Syria au bahari ya Yemen, hapana bali kutoka upande wa Mashariki. Hakika ni upande wa Mashariki, hakika ni upande wa Mashariki." Akaashiria kwa mkono wake upande wa Mashariki."

 

Akasema Faatwimah bint Qays (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) "Nikayahifadhi haya kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).”

 

 

Imaamu na ‘Ulamaa wamekiingiza kisa hiki ndani ya vitabu vyao katika milango ya sifa za Tamiym (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kama alivyofanya Ibnu Hajar katika kitabu chake Al-Iswaabah 1/368 na katika Fat-hul Baariy 12/46 na Imaam An-Nawawiy katika Sharh ya Muslim.

 

 

Amesema Ibnu Hajar katika Al-Iswaabah: "Ni mashuhuri miongoni mwa Swahaba, alikuwa katika dini ya Manasara akenda Madiynah kusilimu."

 

 

Juu ya kuwa kuwemo Hadiyth hii ndani ya Swahiyh Muslim inatosheleza kulazimika kuikubali, kutokana na daraja yake na namna umma wote wa Kiislamu ulivyozipokea Hadiyth zake. Na wapokezi wote wa Hadiyth hii ni watu wenye kuaminika, hapana hata mmoja kati yao mwenye kutuhumiwa, hata hivyo Hadiyth hii imesimuliwa pia na Imam Ahmad na Abu Ya'ala na Ibnu Maajah, na Abu Daawuud, na imepokelewa pia kwa njia ya Swahaba wengine wasiokuwa Faatwimah bint Qays (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kama vile Abu Hurayrah na Mama wa Waumini ‘Aaishah na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ikiwa ni dalili ya kupokelewa kwa njia mbali mbali na wingi wa njia zake, kwa sababu Hadiyth hii haikutolewa na Imaam Muslim peke  yake na wala haikusimuliwa na Faatwimah bint Al-Qays peke yake.

 

 

Amesema Al-Haafidh (Allaah Amrehemu) katika Al-Fat-h (13/323): 

 

 

"Wamekubaliana kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapokubali linalotendwa au kutamkwa mbele yake asilipinge ni dalili kuwa jambo hilo linajuzu, kwa sababu hawezi kukubali kitendo au neno la uongo au kitendo baatil."

 

 

Ama kudai kuwa haya si katika mambo ya dini ambayo Rusuli haijakingwa katika kumsadiki mtu muongo, hilo si kweli, kwa sababu vipi jambo kama hili linalohusiana na dalili za Siku ya Qiyaamah na Imani juu ya Siku ya Mwisho liwe si katika mambo ya yanayohusiana na dini.

 

 

Isitoshe, kama aliyohadithia Tamiym (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni kisa cha uongo ingewezekana kweli wahyi usiteremshwe kukikanusha kisa hicho na kuubainisha ukweli wake, kama ilivyowahi kutokea mara nyingi wakati wanafik na wenzao walipokuwa wakisema kinyume na waliyoficha nyoyoni mwao, na wahyi ukawa unateremka kuwafedhehesha na kubainisha uongo wao?

Juu ya kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) keshahadithia mara nyingi juu ya Ad-Dajjaal na kuteremka kwa ‘Iysa bin Maryam (‘Alayhis-salaam) katika zama za mwisho akihukumu kwa uadilifu kwa kutumia sheria ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa mikono yake atamuua Ad-Dajjaal.

 

 

Yote haya yamesimuliwa kwa njia nyingi sana katika Swahiyh mbili [Al-Bukhaariy na Muslim] na katika vitabu mbali mbali vinavyoaminika. Kwa hivyo habari za dalili ya kukaribia kwa Siku ya Mwisho hazikusimuliwa na Tamiym peke yake (Radhwiya Allaahu ‘anhu), isipokuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliitumia fursa pale Tamiym alipohadithia kisa chake ili awabainishie watu kuwa aliyokuwa akiwaelezea ni kweli na uhakika usio na shaka.

 

 

Hata kama tutachukulia kuwa Hadiyth hii ni katika Israiliyaat, basi ni katika zile sahihi zinazokubalika ambazo tunapaswa kuzikubali kutokana na kukubaliana na sheria yetu.

 

 

Dalili ya maneno haya ni kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: "Na amenihadithia Hadiyth inayokubaliana na niliyokuwa nikikuhadithieni juu ya Masiyh Ad-Dajjaal…"

 

 

Na Wengi Katika Wafasiri Wameitafsiri Kauli Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِّنَ الْأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ أَنَّ النَّاسَ كَانُوا بِآيَاتِنَا لَا يُوقِنُونَ ﴿٨٢﴾

82. Na itakapotimizwa kauli dhidi yao, Tutawatolea mnyama atembeaye katika ardhi atakayewasemezesha kwa sababu watu walikuwa hawana yakini na Aayaat (na ishara) Zetu. [An-Naml – 82]

 

 

Wanasema kuwa myama huyo ni huyu Al-Jassaasah aliyetajwa katika Hadiyth ya Tamiym, kama ilivyosimuliwa na Abdullaah bin ‘Amru. Ikiwa ni hivyo, basi Aayah hiyo ni dalili ya kuisadikisha Hadiyth hii, hasa kwa vile aya haikanushi kuwepo kwake mnyama huyo kabla ya Siku ya Qiyaamah, kwa sababu inaelezea juu ya kutokea kwa mnyama na si kuwepo kwake. Kwa hivyo anaweza kuwepo kabla ya haya.

 

 

Kwa kumaliza tunasema kuwa Hadiyth ni Swahiyh, na inazipa nguvu Hadiyth za Ad-Dajjaal na zile za dalili ya kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah.

 

 

Kwa hivyo kumtuhumu Tamiym (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni muongo na kwamba kaja kuuchafua Uislamu ni tuhuma mbaya kwa Sahaba huyu mtukufu (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye sira yake inashuhudia kuwa ni mcha Allaah na mwingi wa kufanya ‘ibaadah na wema, bali ni kumtuhumu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na ujumbe wake, na hili linatosha kuwa ni dhambi kubwa na uovu ulio dhahiri.

 

 

 

 

Share