Wanaogopa Kuvaa Hijaab Wasije Kufelishwa Mitihani

 

Wanaogopa Kuvaa Hijaab Wasije Kufelishwa Mitihani

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

A.a.

 

Kwanza napenda kuwapongeza kwa kuelimisha jamii kupitia website hii. Napenda kuuliza swali lifuatalo. Mimi ni mwanafunzi nasoma nje ambapo chuoni (university) kwetu miaka mingi tulikuwa haturuhusiwi kuvaa hijabu wasichana kutokana na sheria ya nchi, ila sasa hii sheria wameiondosha tunaruhusiwa ila walimu wetu wengi wanapinga na kutokana na pingamizi za walimu hawa sie tunaogopa kuvaa hijabu tukiwa darasani kwa kuhofia kufelishwa...je hukmu yetu nini??? Na sisi kama waschana tunatarajia kuwa wasomi na kuendeleza jamii yetu ya kiislaam. Naomba ushauri wenu.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

 

 

Tunadhani kulingana na swali lako unaashiria kuwa unasoma Uturuki.  Hakika ni makosa ambao madada wengi hufanya kwa kwenda kusoma katika vyuo ambavyo havimtambui Allaah Aliyetukuka mbali na kwamba wao wenye hizo nchi na vyuo hivyo wanajiita ni Waislamu. Si hayo tu bali wanapigana na kupingana na shariy'ah ya Allaah Aliyetukuka.

 

 

Amri ya Hijaab ni ya kutoka kwa Rabb Muumba ambaye ndiye Mwelewa kwa maslahi yetu hapa duniani. Anasema Aliyetukuka:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ 

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. [Al-Ahzaab: 59].

 

 

Katika amri inayotoka kutoka kwa Allaah Aliyetukuka na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tufahamu kuwa huwa hatuna tena khiyari. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab: 36].

 

 

Hivyo, hilo suala lenu lishaamuliwa khiyari ni yenu sasa mnahofia kufeli hapa duniani au kufeli kesho Aakhirah.

 

 

Mara nyingi huwa sisi tuna khofu kwa jambo lisilokuwepo na lisilo la msingi na tukasahau kuwa Msaidizi wa kihakika ni Allaah Aliyetukuka na si mwalimu wa chuo fulani hapa duniani, mwalimu ambaye mwenyewe ana yake ya kwenda kumjibu Muumba kwa kuchukua madaraka Yake hapa ulimwenguni.

 

 

Ushauri wetu mwanzo ni kuwa maadamu dola yenyewe ishapitisha kuwa mnaweza kuvaa Hijaab chuoni inatakiwa uondoe uoga na ufuate amri ya Allaah Aliyetukuka. Bila shaka, Yeye Atawatolea njia njema kwa Imani yenu.

 

 

Ingia katika kiungo kifuatacho:

 

Kuvaa Nywele Za Bandia Kufunika Nywele Turkey Kwa Sababu Ya Kukatazwa Hijaab

 

 

Tunawaombea tawfiki, istiqaamah na usaidizi kutoka juu, kwa Allaah Aliyetukuka.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share