Kwa Nini Mawe Yataingizwa Motoni

 

Kwa Nini Mawe Yataingizwa Motoni

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

Assalaam Alaykum

Kwanza natoa shukrani zangu za dhati kwa kazi kubwa mnayo ifanya kuelimisha Umma jazaa yenu munitaipata kwa Allaah Amiin.

Swali, Allaah anasema Jahannam kuni zake zitakua Watu na Mawe

- Allaah atuepushe huko Amiin, Kwanini Mawe yataingizwa Motoni - yamefanya kosa gani?

Ahsanteni

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Anaposema Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa kuwa mawe yatakuwa motoni haina maana kwamba mawe yameonewa kuingizwa motoni, kwani mawe sio katika vitu vyenye roho yaani sio viumbe. Bali ni vitu vinavyotumika kupatikana faida fulani kama nyenzo nyinginezo na faida zake mbali mbali.

 

Lakini Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Ametaja katika Aayah ifuatayo kuwa kuni za moto zitakuwa ni watu na mawe kwa vile hao watu walikuwa wakichonga masanamu kutokana na mawe na kuyaabudu. Ndio maana Anasema kuwa Atawaingiza wao pamoja na hayo mawe yao ziwe kama ni kuni za kuchochoea moto wa Jahannam.

إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ ﴿٩٨﴾

Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni vichochezi vya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia. [Al-Anbiyaa: 98]

 

Ibn 'Abbaas  Radhwiya Allaah 'anhumaa amesema  ni : 'kuwaka (moto)' [Al-Qurtubi 11:343]

 

'Kuni za Jahannamu' ina maana kwamba kuni za moto.  Mujaahid, Ikrimah na Qataadah wamesema: "Ni mafuta".  Adh-Dhwahaak amesema: "Mafuta ya Jahannam ina maana ni kile kinachotumbukizwa ndani yake" [At-Twabariy 18:536 – Tafsiyr Ibnu Kathiyr 6:500]Na hii pia ni rai ya wengineo [At-Tabariy 18:536 katika Tafsiyr ya Ibnu Kathiyr 6:500]Na ndio maana pia  Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anasema katika Aayah nyingine,

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa[At-Tahriym  6]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share