Mashairi: Maulidi Walianzisha Mashia

                    Maulidi Walianzisha Mashia

            ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

Salaam Waislamu, kokote ulimwenguni,

Akili zangu timamu, ninasema kwa kanuni,

Nataka munifahamu, muelewe kwa yakini,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia.

Walianzisha Mashia, kundi la Faatwimiyyuni,

Dhehebu Ismailia, Makoja wa Jamatini,

Ni Misri walianzia, sherehe hii ya shetani,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Hakuna bid’aa hasana, ni uzushi mitaani,

Wa “Kullu Bid’atin” dhalaala, ndugu zangu amkeni,

Msichoke kubishana, wanafiki wapingeni,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia.

Na vipi tutafurahi, siku hiyo kumbukeni,

Ni siku alofariki, Mtume wa Rahmani,

Kwa hivyo ni unafiki, kama si hivyo ni nini ?

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia 

Ninasema kwa uchungu, moyoni nina huzuni,  

Mtume wa Wetu adhimu, hakutwambia fanyeni,

Ninawaomba wenzangu, dalili tuonyesheni,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Watu wanakusanyika, na kuimba hadharani,  

Na wengine wanapika, pilao na biriyani,

Ziara inafanyika, usiku kucha jamani,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Hawakufanya zamani, maswahaba Waumini,

Nawaomba zindukeni, ni ujinga akilini,

Kuigiza ya kigeni, kigeni ndani ya dini,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Bid’ah iepukeni, mwisho wake ni motoni,

Tabia hii acheni, Mashekhe waulizeni,

Wakiwaambia fanyeni, muwajibu “samahani,”

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Niliona Makadara, pale Mombasa mjini,

Wasichana kujipara, na manukato mwilini,

Sasa hiyo ni izara, Maulidi aina gani?

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Maulidi nenda Lamu, kajionee machoni,

Hukusanyika Walimu, na majoho mabegani,

Wanakuja Maimamu, na mivilemba vichwani,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Na Unguja kadhalika, na Pemba kila makani,

Watu wanashughulika, faida hatuioni,

Madhambi yanachumika, hawasikii maoni,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Sikukuu ya Taifa, ni Maulidi nchini,

Wala si siku ya sifa, ya Mtume Muhisani,

Hii siku ya maafa, si furaha asilani,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Na “mashekhe” makhaini, Allaah Waweke pembeni,

Allaah Awatie dhiki, akhera na duniani,

Na watu huwasadiki, kama vipofu njiani,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Ulizeni Walosoma, wawatoe mashakani,

Tusiwe kama wanyama, akili za hayawani,

Hatutachoka kusema, ukweli utabaini,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Utaona wanaimba, kwa sauti nzuri hewani,

Sauti ile nyembamba, wanavutia puani,

Na maneno huyapamba, kama vile harusini,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia.

Mtume angekuweko, hakika angewalaani,

Haya yote ni vituko, mapambo ya duniani,

Akhera kuna viboko, na minyororo motoni,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia.

Masufi wameidaka, na wao wamo kundini,

Wao sasa wameshika, na bendera mkononi,

Wapo wanashughulika, kudanganya waumini,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia.

Ukiwapinga hunena, huyu Wahabi oneni,

Hawajui yake maana, huropoka midomoni,

Dalili kwanza hawana, majahili kwenye dini,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia.

Sherehe zetu ni mbili, sherehe toka zamani,

Idd-ul-Fitri awali, baada ya Ramadhani,

Idd-ul-Adh'ha ya pili, mwezi wa Hija yakini,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia.

Na moto kwenye chetezo, na kufukiza ubani,

Ulikuwa ni mchezo, wa Mafursi wa Irani,

Ni mwisho wa maelezo, nawaaga ikhwani,

Happy Birthday Maulidi, walianzisha Mashia

Share