Mema Na Mabaya Yameumbwa Na Allah?

SWALI:

Asalam aleikum,

Je, Allah (swt) Aliumba uzuri (good) na ubaya (evil) ama aliumba uzuri pekee na ubaya unatokea kwa sababu watu wanapotezwa na shetani mpotevu. Tafadhali niongoze

 

 


 

JIBU:

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa ndugu yetu aliyeuliza swali hili zuri kuhusu utukufu wa Allah na uwezo Wake na utendaji kazi Wake. Hakika ni kuwa Yeye haulizwi anayoyafanya lakini sisi ndio tutaulizwa kwa yote tunayo yafanya hapa duniani na Atatulipa Pepo kwa mema na kutuadhibu na Moto kwa maovu tunayo yatenda. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliumba viumbe, mbingu, ardhi na vitu vyenginevyo. Vitendo vibaya au vizuri vinatokana na ule uhuru tuliopatiwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala). Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatuelezea kuwa Ametupatia viungo vya kutusaidia ili kumuabudu Yeye peke na kumtumikia, kumtii na kumnyenyekea. Anasema:

Hakika Sisi Tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru” (76: 3).

Na tena:

Kwani hatukumpa macho mawili? Na ulimi, na midomo miwili? Na Tukambainishia zote njia mbili?” (90: 8 – 10).

Anatuelezea tena:

Na Tumeiumbia Jahanamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika” (7: 179).

 

Hivyo, mwanadamu ndiye mwenye kufanya hayo maovu na mazuri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share