Kusengenya (Ghiybah) Japo Kuwa Anayesengenywa Anayo Sifa Yenyewe Ni Dhambi

SWALI:

Tunasikia kuna Hadiythi inasema ukimsema mtu ni mfupi au mrefu ni vibaya! nami sikusema hivyo kwa kumdharau bali nimeuelezea wasifu wake jinsi alivyo, naomba ufafanuzi?

 


JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Muislam haruhusiwi kuichafua heshima ya mwenzie kwa kumkashifu mbele ya watu wengine, sawa ikiwa unachokisema kina ukweli au kinyume chake.

Hata ikiwa mtu anayo sifa ile lakini madamu unamsema nyuma yake na ni jambo ambalo mwenyewe asingelipenda kulisikia basi pia huingia katika hukmu hii ya ghiybah:

 

  عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ :  (( أَتَدْرُونَ مَا الْغِيبَةُ ؟ )) قَالُوا : اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ ، قَالَ :   ((ذِكْرُكَ أَخَاكَ بِمَا يَكْرَهُ )) ، قِيلَ : أَفَرَأَيْتَ إِنْ كَانَ فِي أَخِي مَا أَقُولُ ؟ قَالَ :  (( إِنْ كَانَ فِيهِ مَا تَقُولُ فَقَدِ اغْتَبْتَهُ ، وَإِنْ لَمْ يَكُنْ فِيهِ فَقَدْ بَهَتَّهُ)) [ أخرجه مسلم ]

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) kwamba aliuuliza Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa alihi wa sallam): ((Je mnajua maana ya Ghiybah? [Kusengenya])) Wakasema: Allah na Mjumbe Wake wanajua. Akasema: ((Ni kumtaja ndugu yako kwa jambo analochukia)). Akaulizwa: Hebu nieleze, iwapo ndugu yangu anayao yale niyasemayo? Akasema: ((Ikiwa analo hilo usemalo basi umeshamsengenya, na ikiwa hana hilo usemalo basi umeshamzushia uongo)) [Muslim]

 

 Bibi ‘Aaishah alisema: “Nilimuambia Mtume Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam:

  "حسبك من صفية كذا وكذا"، قال بعض الرواة: تعني قصيرة، فقال: (( لقد قلت كلمة لو مزجت بماء البحر لمزجته))  

“Acha (kumsema) Swafiyah kadhaa na kadhaa” [katika riwaaya nyingine yaani ni mfupi] Akasema (Mtume Swalla Allahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) ((Umesema neno ambalo lingelichanganywa na maji ya bahari lingeichafua)) [Abu Daawuud na At-Tirmidhiy]

Kumsengenya mtu nyuma yake (Ghiybah) ni dhambi ambazo hazisamehewi na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hadi mwenyewe uliyemsengenya akusamehe kwani hiyo ni katika haki za baina ya binaadamu. Ama haki za baina ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) na mja Wake, Yeye Humsamehe pindi anapoomba toba. Na jambo hili la haki za baina yetu limekuja makatazo yake katika Aayah zifuatazo:  

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَومٌ مِّن قَوْمٍ عَسَى أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاء مِّن نِّسَاء عَسَى أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ بِئْسَ الاِسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ))

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ وَاتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ))

((Enyi mlioamini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasiotubu, hao ndio wenye kudhulumu))  

 

((Enyi mlioamini! Jiepusheni sana na dhana, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anayependa kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Allah. Hakika Allah ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu)) [Al-Hujuraat: 11-12]

 

Hivyo haifai kabisa kumvunjia heshima ndugu mwenzio au kumsengenya. Makatazo haya pia yamekuja katika mafunzo ya Mtume (Swalla Allah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

عن أنس قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم (( لما عرج بي مررت بقوم لهم أظفار من نحاس يخمشون وجوههم وصدورهم، فقلت: من هؤلاء يا جبريل؟)) قال: هؤلاء الذين يأكلون لحوم الناس ويقعون في أعراضهم"

Kutoka kwa Anas (Radhiya Allahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Nilipopandishwa mbinguni (Siku ya Israa na Mi’raaj) nilipita kwa watu ambao walikuwa wana kucha za shaba nyeupe wakijichana nyuso zao na vifua vyao. Nikauliza: Nani hawa ewe Jibriyl? Akasema: Hawa ni watu ambao wamekula nyama za binaadamu na kuwavunjia heshima zao)) [Abu Daawud]

 Na Allah Anajua zaidi

 

Share