Wepi Ni Wajibu Kuwahudumia Kwanza, Wazazi Au Mke Na Watoto?

 

Wepi Ni Wajibu Kuwahudumia Kwanza, Wazazi Au Mke Na Watoto?

 

Alhidaaya.com

 

Swali:      

 

 

Assalam Aleykum Warahamtullah Wabarakatuh,

 

Kwanza nitoe shukran zangu za dhati kwa jawabu la suala langu lililopita na nimekinai na jawabu lako.  Hivyo nimevutiwa kuja tena kwa faida yangu na umma wa kiislam. Napenda kupata ufafanuzi juu ya wajib wa mtoto kwa wazazi wake. Ikiwa kiuchumi mtoto ambae ana familia inayomlazimu kuikimu, kwa maana ya mke na watoto na kipato chake si cha kutosheleza na wazazi pia hawajiwezi vya kutosha jee mtoto huyu atizame wale waliondani ya nyumba yake au atimize wajibu wa wazazi kwanza na pindipo ikiwa ipo ziada na atizame watoto wake?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Kuwafanyia wema wazazi wawili na kuwapa umbele katika hili ni jambo lililosisitizwa na Uislam, hata ikafikiwa kuwa miongoni mwa amali –tawassul- ya mja ya kujikurubisha mbele ya Allaah ni kuwafanyia wema wazazi wake kama ilivyothibitika katika Hadiyth ya wale watu watatu waliofungiwa katika pango na kila mmoja akataka msaada wa Allaah Aliyetukuka kwa kuomba kupitia kwa amali njema alizofanya. Na kwa wema aliowafanyia wazazi wake Allaah Aliyetukuka Akakubali na kuwapatia tahfifu na kuwafungulia pango hilo. [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Hii inaashiria kuwa kuwatanguliza wazazi kwa huduma yoyote ile kabla yako binafsi wachilia mbali watoto wake ndio hasa linalotakiwa kama unatafuta radhi na malipo kutoka kwa Allaah, kwani Allaah Amewajibisha juu yako mtoto uwafanyie wema na ihsaan wazazi wako- utimize wajibu wa wazazi kwanza na pindipo ikiwa ipo ziada ndio tazama nafsi yako na mkeo na watoto wake – mpaka Ameliambatisha jambo hilo na haki Yake Allaah pekee ya kuabudiwa, kama inavobainika katika Aayah hii:

 

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾

Na Rabb wako Amehukumu kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima. [Al-Israa: 23.]

 

 

Na asli katika kuwafanyia wema wazazi wawili ni Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amru bnul ‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) aliposema:

 

 

"Alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia nakuahidi kuwa nitafanya Hijrah na kupigana Jihaad natarajia malipo kutoka kwa Allaah; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: Je, yuko katika wazazi wako wawili aliye hai? Akajibu: Na’am, wote wawili wako hai. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Unataka malipo kutoka kwa Allaaah? Basi rejea kwa wazazi wako wawili na uwafanyie wema” [Imepokelewa na Muslim, kitabu kuwafanya wema na kuunga na adab, mlango wa kuwafanyia wema wazazi wawili na kuwa wao wawili ndio wenye kustahiki kufanyiwa wema.]

 

 

'Ulamaa wanasema kama wazazi hawajiwezi basi ni wajibu wa mtoto wao kuwatazama na kuwatimizia haja zao kadiri ya uwezo wake –bila ya taklifa- kwa kilicho kizuri kuliwa na mtu ni kile alichokichuma mwenyewe, na mtoto wake –alichochuma mtoto wake- ni katika chumo lake.

 

 

Ndio ikawa kuchukuwa wazazi chochote katika mali ya mtoto wao kiasi cha haja yao na mahitaji yao inajuzu hata kama hakuidhinisha huyo mtoto wao.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share