Maulidi: Ikiwa Qur-aan Imehifadhiwa Vipi Swahaba Walikhofia Kupotea? Maulidi Yana Ubaya Gani?

 

Maulidi: Ikiwa Qur-aan Imehifadhiwa Vipi Swahaba Walikhofia

Kupotea? Maulidi Yana Ubaya Gani?

 

Alhidaaya.com

Swali:

 

mimi hupendezwa na malumbano ya ki-ilmu na hupeda kuchangia kidogo dogo.Hoja ya 9 imelemea zaidi katika khofu ya kupotea Quran baada ya maswahaba wengi waloihifadhi moyoni kufa vitani (khofu ya nini, na Allah keshasema Nahnu Nazzalna Dhikra, Wa-Inna Lahu Lahaafidhuun). Je, nao wakumbukao mazazi ya Nabiy kwa kutumia kigezo cha khofu ya kusahaulika Nabiy kwavile dunia yetu hii imeharibika sana kwa mambo na anasa nyingi pamoja na mbio ziso julikana, watakuwa sawa?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam  zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Qur-aan iko wazi kuwa kama mtu anayo dalili kwa madai yake basi na alete hiyo dalili kama ni msema kweli:

... هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١١١﴾

Leteni ushahidi wenu wa wazi mkiwa ni wakweli. [Al-Baqarah: 111]

 

Hivyo basi ndugu yetu, tunapenda tuelewe kuwa katika Uislaam hakuna malumbano- mabishano – bali kuna majadiliano tena kwa namna iliyo bora kabisa kulingana na watu unaojadiliana nao; wenye vyeo jadiliana nao kwa maneno ya hikima kwa mujibu wa akili zao; watu wa kawaida walinganie kwa kuwapa mawaidha yanao waelekea, na kuwapigia mifano ya mambo wanayopambana nayo ya kuwapeleka kwenye Haki; na watu wa dini zilizotangulia katika watu waliopewa vitabu au wenye kudai kuwa wanafuata vitabu vilivyotangulia Mayahudi na Manasara, jadiliana nao kwa kutumia hoja za kiakili, Mantiqi, na maneno laini, na majadiliano mazuri; si malumbano wala maneno ya ukali na matusi, ili uwakinaishe na uwavutie.

 

Hii ndiyo njia ya mjadala kama uko katika Uislamu, mjadala wenye kubeba dalili zilizo wazi mjadala wa kielimu mjadala wa kuwakatika watu kila la kheri na sio malumbano ambayo umesema: 'mimi hupendezwa na malumbano ya ki-ilmu'; kwani malumbano huwa si ya kielimu kwani ni mabishano jambo linaloweza kumpelekea mtu kukataa haki kwa sababu za kibinafsi na sio vyengine; na Muislamu hutakiwa afuate haki hata kama haki hiyo anayo adui wake maadamu ni haki basi unatakiwa umuunge mkono huyo adui wakati huo kwa kuwa alichokisema ni haki.

 

Si katika kawaida ya Muislamu kutaka au kupenda kuwa kama hivyo ulivyosema,  'hupeda kuchangia kidogo dogo' hasa akielewa kuwa dini ya Kiislamu si dini iliyotungwa na watu kama vile katiba ya chama au nchi bali ni dini iliyoteremshwa na Al-Hakiym Al-Hamiyd; hivyo basi huna haja ya kuwa na ushabiki wala kutaka kuchangia kitu katika dini wala kupendekeza waulize wenye elimu kama jambo hulielewi na wao In shaa Allaah kwa tawfiki yake Rabb watakutosheleza na kukuondoshea kiu chako kwa yale waliyotunukiwa na Al-Hakiym Al-Hamiyd kama inavyoshauri Qur-aan:

... فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ﴿٤٣﴾

Basi ulizeni watu wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui. Kwa hoja bayana na vitabu. Na Tumekuteremshia Ukumbusho (Qur-aan) ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao huenda wakapata kutafakari. [An-Nahl: 43-44]

 

Hivyo basi hatutakiwi tuchangia kwani hakuna cha kukichangia dini imekamilika tokea wakati wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kama kitu huelewi basi uliza wenye elimu wakufunue macho badala ya kuleta mawazo na fikra zako pahala pasipohitaji hayo yote.  Allaah Anasema:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾

Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Al-Hijr: 9]

 

Aayah inathibitisha kuwa Allaah Amechukuwa jukumu la kuilinda Qur-aan isiingiliwe na mageuzo na mabadiliko yoyote –angalia maelezo mafupi ya tafsiri ya al-Farsi kuhusu hili neno kuilinda Qur-aan- mpaka kusimama Qiyaamah; hivyo basi Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliposhauriana na kukubaliana kuikusanya Qur-aan yote na kuiandika pahala pamoja si kuwa walikuwa kama ulivyosema  wana ‘khofu ya kupotea Qu-raan baada ya Swahaba wengi waloihifadhi moyoni kufa vitani’ kwani wao hawakuelewa haya ‘Nahnu Nazzalna Dhikra, Wa-Inna Lahu Lahaafishuun’ kinadharia; bali waliyaelewa haya ki Iymaan na kiitikadi na si hivyo tu; bali wao walikuwa na yakini isiyokuwa na chembe ya shaka kuhusiana na Alichokisema Ar-Rahmaan na hivyo ndiyo tunavyotakiwa sisi Waislamu tuwe.

 

Hivyo basi khofu yao haikuwa 'ya kupotea Qu-raan' bali ilikuwa katika kupotea Qurraa (wasomaji) na Huffaadh (waliohifadhi) Qur-aan na kupotea kwao huenda kukasababisha kupotea kwa ufundishaji wa Qur-aan kupotea visomo vya Qur-aan kama walivyofundishwa na kusomewa na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na si kupotea kwa kilichohifadhiwa na Mwenye uwezo wa kweli kweli na wa uhakika wa kuhifadhi naye si mwengine isipokuwa Allaah.

 

Na nani anaweza kukataa kuwa huku kukubaliana kwa Swahaba wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuikusanya na kuiandika Qur-aan pahala pamoja kuwa si katika ilhaam yake Rabb kwao kufanikisha ‘amali hiyo na huenda pia ikawa ni miongoni mwa namna nyengine ya ar-Rahmaan kuilinda Qur-aan

 

Sahaba wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walielewa kuwa Qur-aan ishakamilika na hakuna kitachokuja kufuta hukumu naasikh na kitakachofutwa mansuukh kwani Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayupo na hivyo hakuna kushuka Qur-aan tena, na ‘ahdi ya Kuja Jibriyl imemalizika kwa kumalizika kwa maisha ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivyo khofu yao si kupotea Qur-aan bali kupotea Maqurraa wa hiyo Qur-aan.

 

Umesema, 'Je, nao wakumbukao mazazi ya Nabiy kwa kutumia kigezo cha khofu ya kusahaulika Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa vile dunia yetu hii imeharibika sana kwa mambo ya anasa nyingi pamoja na mbio ziso julikana, watakuwa sawa?' Ukweli ni kuwa hiki ni kigezo kisichokuwa na muwafaka wa aina yo yote ile –Qiyaas mal Faariq-; kwani si katika fikra wala mawazo ya Muislamu wa kawaida achilia mbali wenye kuelewa Uislamu na kuufuata kwa kushikamana nao katika maisha yao ya kila siku kufikia kwa kweli ni muhali ni jambo lisilo wezekana kwa Waislamu kufikia kumsahau aliyekuwa akihuzunishwa kwa yanayowataabisha; akiwahangaikia sana, tena ni mpole na mwenye huruma sana kwa Waislamu kuliko mama kwa mwanawe.

 

Vipi watafikia kumsahau Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Vipi watafikia kumsahau wanayetakiwa kumpenda kuliko wanavyowapenda ahli zao, watoto wao, na watu wote?

 

Kumtaja kwao yeye ikiwemo ndani ya Swaalah zao, du’aa zao, kumfuata/ kigezo katika kila kipengele cha maisha yao ya kila siku ikiwemo kula kunywa kuvaa nguo kuzivua n.k. Pamoja na kumswalia kila akitajwa hutakiwa tumswalie na kama hakutaja ni katika ‘ibaadah aliyotuwekea Rabb kumswalia, kadhalika kumfanya kuwa muamuzi katika mambo yetu yote na kuwa radhi na uamuzi wake, kumuenzi, kumnusuru na kadhalika

 

Kwa hali hizo zote tulizotaja kweli tunaweza kumsahau Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) 'kwa vile dunia yetu hii imeharibika sana kwa mambo na anasa nyingi pamoja na mbio ziso julikana,' huku tukielewa bali tukiwa na yakini kuwa tutaiaga hii dunia?!  Vipi ‘watakuwa sawa? wale wanaojua na wale wasiojua? Vipi watakuwa sawa? watu wa Motoni na watu wa Jannah (Peponi)? Na hali watu wa Peponi ndio wenye kufuzu? Vipi tutaweza kufikia kumsahau atakayesimama kutuombea mbele ya ar-Rahmaan?!  Ni kweli visingizio hivi na vyengine kama hivi vitaweza kupelekea Waislamu kumsahau aliye letwa kwao ambae Qur-aan inamueleza kama:

 

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا ﴿٢١﴾

Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi. [Al-Ahzaab: 21]

 

Hivyo basi  kama ulivyosema kuwa, ‘wakumbukao mazazi ya mtume kwa kutumia kigezo cha khofu ya kusahaulika Nabiy (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam)' Hao ndugu yetu wanatakiwa waelewe kuwa kumsahau Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni sawa na kuisahau dini yote na hili haliwezekani mustahili!

 

Hivyo basi hakuna haja ya kukumbuka mazazi yake kwa kuwa hilo halina cha kutupeleka kumkumbuka Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haliwezi kuondosha khofu -kama ipo ya kusahauliwa yeye- na kitachoweza kuthibitisha kuwa tunamkumbuka ni kushikamana na mafundisho yake katika maisha yetu ya kila siku mpaka itufikie yakini na kuomba tawfiki ya ar-Rahmaan kuweza kututhibitisha kwa kujibu suala katika kaburi kuwa  Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni Rasuli wa Allaah na tulimfuata kama tulivyotarajiwa na Mola kwa tawfiki yake Rabb.

 

Kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kikweli ni kumfuata kwa aliyokuja nayo na kuachana na ambayo hakuyafanya, hakuyaamrisha, hakuyaridhia, wala ambayo hakufanyiwa na wapezi wake wakubwa kama kina Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Hakika wao walikuwa na mapenzi makubwa kwake na hawakulijua hili la kumsherehekea siku ya kuzaliwa wala hawakulifanya.

 

Ama sisi mapenzi yetu ni ya kujionyesha na vitendo vyetu vinatusuta.

 

In shaa Allaah Allaah Atatuhidi katika mapenzi ya kweli yenye kuthibitishwa na vitendo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share