Kualika Watu Kusoma Qur-aan Kuomba Haja

 

 Kualika Watu Kusoma Qur-aan Kuomba Haja

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalam aleikum,

 

Tunavyojua katika jamii yetu kuwa mtu akifariki huwa anasomewa hitma na humo watu wanasoma dua pamoja,  pia huchinjwa mnyama kwa ajili ya sadaka yake. Je mnasemaje mashekhe wetu hivyo ndivyo sawa?   Yepi yanayomfaa mzazi kumfanyia baada ya kufariki? Naomba jibu mashekhe wetu kwani mengi mmetufunza ya haki tumeelimika na kutoka ujingani wa kufuata tu mambo yasiyo katika dini. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) awalipe juhudi zenu.

Asanteni sana.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mambo haya yenye utata yameenea kwa wengi hasa katika maeneo yetu ambayo jambo hili ni ada na desturi. Kwa asiyefanya huonekana ni mtu wa ajabu na labda huenda amekuja na Dini mpya. Tufahamu kuwa masharti makuu ya ‘Ibaadah yoyote katika Dini yetu Tukufu, Uislamu ni:

 

1.  Ikhlaasw

 

2. Kufuata kama ilivyopokelewa katika Sunnah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

 

Likikosekana sharti moja kati ya haya mawili basi ‘Ibaadah hiyo huwa haijakamilika na hakuna thawabu yoyote kwa 'amali aliyofanya mja.

 

Kuhusu Du‘aa, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Du‘aa ni ‘Ibaadah." [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ibn Hibbaan na Al-Haakim].

 

Yapo mambo muhimu ambayo yanapofanywa yatamnufaisha maiti wako hasa akiwa mzazi wako (mama au baba au wote wawili).

 

Ama khitmah, kisomo cha pamoja na Du‘aa ya pamoja si katika mambo hayo yatakayomnufaisha maiti. Hii ni kwa kuwa haya yote hatukuyapata kutoka katika mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ama Du‘aa, hakika hilo ni jambo muhimu kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatueleza kuwa Waumini wanatakiwa waombeane Du‘aa na hizo huwa zinanufaisha ndugu zao ambao wametangulia. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٠﴾

Na wale waliokuja baada yao wanasema: Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. [Al-Hashr: 10].

 

Mambo ambayo yanamfaa maiti ni mengi. Miongoni mwayo ni:  

 

1. Kumuombea du‘aa moyoni kwa kila aliyehudhuria kaburini baada ya kuzikwa. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Muombeni Allaah Amsamehe ndugu yenu na amfanye thabiti kwani hivi sasa anahojiwa" [Abuu Daawuwd].

 

2. Kumswalia Swalaah ya jeneza anapoaga kwa mujibu wa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Hakuwa Muislamu aliyekufa na watu wakasimama katika jeneza lake wakafikia arobaini hawamshirikishi Allaah na chochote ila Allaah Atakubali maombezi yao." [Muslim]. Lakini ni ajabu leo hata jamaa wa karibu wa maiti hawamswalii maiti wao Swalaah hii ya jeneza bali hungoja nje ya Msikiti baada ya kuswaliwa na ndio wakachukua jeneza la mtu wao. Vipi maiti atapata fadhila kama hizo?

 

3. Kumlipia funga alizokosa maiti wako. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Atakayekufa ilhali kaacha deni la funga basi alipiwe na walii wake." [Al-Bukhaariy na Muslim]. Walii ni mtu wa karibu wa aliyekufa, kwa mfano mtoto kwa wazazi wake au kinyume chake au warithi wa maiti huyo.

 

4. Kumlipia nadhiri ikiwa alinadhiria na akafa kabla ya kuitekeleza.

 

5. Kumtolea sadaka. Mtu mmoja alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Mama yangu alijisahau na lau angeliweza kusema angetoa sadaka; je, atapata ujira nikimtolea sadaka?" Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu: "Ndio atapata ujira na malipo kwa sadaka hiyo." [Al-Bukhaariy na Muslim]. Hivyo, kumtolea maiti wako ipo na katika hilo unaweza kuwalisha kuwavisha mayatima, masikini na mafakiri, kutoa mali kwa kuwasaidia au kuchinja na kugawa nyama kwa wanaostahiki na maiti atapata ujira wake kwa hilo.

 

6. Kumhijia ambaye hakupata nafasi ya kuhiji. Ikiwa una wasaa wa kifedha nawe ushatekeleza 'amali ya Hijjah unaweza kumhijia mtu wako ambaye hakupata fursa na thawabu zitamwendea.

 

Mwanamke mmoja kutoka katika kabila la Juhaynah alikwenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Mama yangu aliweka nadhiri kuwa atahiji lakini hakuhiji hadi alipofariki; je, nimhijie?” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: “Ndio, mhijie. Je, huoni kuwa kama mama yako angekuwa anadaiwa ungemlipia deni lake? Tekeleza deni la Allaah na yeye ndiye Mwenye haki zaidi ya kulipwa deni Lake.” [Al-Bukhhariy].

 

7. Kijana mwema atakayemuombea Du‘aa. Wewe kijana ndiye mwenye jukumu la kumuombea mzazi wako na si kukodisha watu kwa kufanya zoezi hilo. Ni ajabu kuwa mtu atatoa pesa ili kwenda kinyume na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na maiti wake asipate chochote ilhali yeye anaweza kumpatia mzazi wake thawabu bila ya gharama yoyote. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾

Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni. [Al-Israa: 24].

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Atakapokufa mwanadamu matendo yake yote hukatika ila kwa mambo matatu: Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye kunufaisha au kijana mwema atakayemuombea Du‘aa." [Muslim].

 

Dini yetu ni nyepesi na inamtakia kila mja aweze kutekeleza 'amali zake kwa urahisi, lakini pindi tunapoanza kuzua na kuongeza yasiyokuwemo na yasiyo katika mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum), basi bila shaka, mambo yatakuwa mazito na yasiyo na ujira wowote mbele ya Allaah.

 

Hivyo, kuwakusanya watu kwa ajili ya du‘aa haifai wala haimsaidii maiti wako, na isitoshe ni taklifa na ubadhirifu wa mali.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share