Mashairi: April Fool Ni Uongo Na Uongo Ni Haramu

April Fool Ni Uongo Na Uongo Ni Haramu

‘Abdallah Bin Eifan

(Jeddah, Saudi Arabia)

Salaam kwa ndugu zangu, nawaombea uzima,

Namuomba Mola wangu, tuishi kwa usalaama,

Vituko vya ulimwengu, vimezidi kutuuma,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Na uongo ni haramu, dini yetu imesema, [An-Nahl: 105]

Mwenye akili timamu, anasema kwa hekima,

Si kama mwendawazimu, husema bila kupima,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Hivi si kutaniana, uongo si kitu chema,

Mwisho ni kutukanana, kuvunjiana heshima,

Au hata kupigana, kama mfano wanyama,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Utani huo hatari, una madhara kwa umma,

Ukitangaza habari, za uongo zikavuma,

Matokeo si mazuri, moyo waweza simama,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Habari ya kushtua, na khasa kwa kina mama,

Inaweza ikaua, pia kwa watu wazima,

Lawama utachukua, na madhambi kuzichuma,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Makafiri kuwaigiza, imekua ni kilema,

Wao wametupoteza, wanataka tuwe nyuma,

Ili tuwe kwenye kiza, wapo wanatuandama,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Sababu zake kwa kweli, bado hatujazisoma,

Sababu tusizijali, mwisho wake ni lawama,

Tusifuate majahili, mwisho watatusakama,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Mambo mengi ya kigeni, huku kwetu wanatuma,

Mother Day tazameni, eti kumbusho la mama,

Mama kwenye yetu dini, anakumbukwa daima,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Au siku ya “mapenzi”, Valentina tazama,

Nyekundu wanaienzi, eti ndio ni alama,

Kumbe yote ni upuuzi, shetani hutusukuma,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Shetani anakazana, tuwe kwenye chake chama,

Si usiku si mchana, yupo hakati tamaa,

Kamtoa Subhana, katika Yake rehema,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Uongo ni wa shetani, hudanganya akisema,

Hutupambia machoni, mabaya hufanya mema,

Tuwe pamoja motoni, moto unapotuchoma,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Adui wetu mkubwa, shetani hana huruma,

Mtihani ni mkubwa, kupambana na dhuluma,

Na Mola wetu Mkubwa, Katupa kila neema,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Mashekhe wanahubiri, wanafanya kila hima,

Wanafuata zile amri, za Mola wetu Karima,

Hakuna cha kusubiri, lini watu watakoma?

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Tukae tukifikiri, dunia tutaihama,

Tuikumbuke kaburi, tukumbuke na Qiyama,

Hapa nafunga shairi, kalamu imeshakwama,

April Fool ni uongo, na uongo ni haramu.

Share