Mashairi: Mirungi Majani Ya Mashetani

                ‘Abdallah Bin Eifan

             (Jeddah, Saudi Arabia)

Salaamu zangu narusha, angani na ardhini,

Napenda kuwakumbusha, kuhusu haya majani,

Mirungi inavyotisha, kwa madhara ya mwilini,

Majani ya mashetani, mirungi  nawakumbusha.

Mirungi nawakumbusha, majani ya mashetani,

Mirungi  inasumbusha, chakula hukitamani,

Usingizi inarusha, upo macho taabani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Akili inazungusha, kama mwehu barazani,

Mashavu inavimbisha, kama pulizo yakini,

Mawazo ya kupotosha, yanakujia kichwani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

“Nakhwa” inapandisha, majasho tupu usoni,

Wakati inapitisha, wala faida huoni,

Maradhi husababisha, na magonjwa ya tumboni,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Haina haja kubisha, wamo pia wanandani,

Wasichana hujitwisha, na mirungi mikononi,

Upate kumridhisha, mnunulie sokoni,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Usiku anavyokesha, kama bundi wa porini,

Hungoja kwenye dirisha, mke yupo dirishani,

Lini bwana atabisha, mlango apite ndani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Uongo wanavumisha, eti “akher” hutamani,

Na kumbe hudhoofisha, uume wake wa chini,

Yote ni kubabaisha, atamdanganya nani ?

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Hapo anakorofisha, “uhusiano” chumbani,

Na mke anapandisha, apandapo kitandani,

Na mume ameshakwisha, hafai tena jamani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Inaharibu maisha, hukufanya tafrani,

Sana inahangaisha, ukikosa mdomoni,

Tafuta wa kukopesha, hana pesa mfukoni,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Anashindwa kujilisha, lakini yupo mbioni,

Ona hujidhalilisha, anaomba masikini,

Mdomo unamwasha, hajuwi afanye nini ?

Majani ya mashetani, mirungi nawajulisha.

Watoto hujifundisha, kuanzia utotoni,

Tabu kujirekebisha, wakifika ukubwani,

Hakika yasikitisha, wanakuwa hatarini,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Dini imeharamisha, Mashekhe waulizeni,

Visa vyake vinatosha, kuiita maluuni,

Watu hujikalifisha, huleta shida nyumbani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Mirungi wanaotesha, Ethiopia hadi Yemeni,

Na Kenya nawajulisha, ipo Meru milimani,

Halafu husafirisha, kwa ndege kila makani,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Somalia huifikisha, kwa kupitia angani,

Tanzania hupitisha, kwa kuvuka mipakani,

Inawasili Arusha, na kutoroshwa nchini,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Shairi nasimamisha, kwenda mbele natamani,

Wakati umeshakwisha, nakimbilia kazini,

Mungu Atatusafisha, Rehema Zake ombeni,

Majani ya mashetani, mirungi nawakumbusha.

Share