Mashairi: Sifa Njema Ni Za Allaah

Sifa Njema Ni Za Allaah

          ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

Alhidaaya.com

Edita nipe uhuru, niwasalimie umma,

Liruke kama kunguru, shairi langu natuma,

Usinitoze ushuru, nina machahe kusema,

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Tuzidi kumshukuru, ni za Allaah sifa njema,

Kwa Jina Lake Ghafuru, hutimia mambo mema,

Madhambi Ayaghufuru, Aihifadhi neema,

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Shukuru Usikufuru, Subhana Amesema, (Al-Baqarah:152)

Muumba Tumdhukuru, leo, kesho na daima,

Kwa ulimi tushukuru, kwa moyo na mambo mema,

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Azidi kutunusuru, Tumshukuru lazima,

Azidi kutupa nuru, hapo siku ya Qiyaama,

Shetani asitudhuru, tusiwe kama wanyama,

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Ona Amesema nini, Mola wetu Rahmani,

Wale wenye shukurani, huongezewa yakini, (Ibrahim : 07),

Na kwa hivyo Waumini, aya tuzingatieni,

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Tusikufuru jamani, tukipewa mitihani,

Tuongeze shukurani, iwe thabiti imani,

Tumshukuru Manani, na tuombe samahani,

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Tushukuru tukinyimwa, tushukuru tukipewa,

Hayuko Anaetowa, ila Yeye Msifiwa,

Riziki Yeye Hugawa, vile Anavyoamuwa, (Ar-raa’d : 26)

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Ninakushukuru Mungu, Kunifanya Muumini,

Ninakushukuru Mungu, Kunipa afya mwilini,

Ninakushukuru Mungu, Kunisitiri nyumbani,

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Ninakhitimu shairi, Namshukuru Qahari,

Atuepushe na shari, na Atupe kila kheri,

Ni mwisho wa msitari, ninafunga daftari,

Ni Za Allaah sifa njema, tuzidi Kumshukuru.

Share