Kumsomea Qur-aan Maiti Kama Suratul-Baqarah Baada Ya Kumzika Inafaa?

 

Kumsomea Qur-aan Maiti Kama Suratul-Baqarah  Baada Ya Kumzika Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaikum,

 

Nataka kujuwa ithibati ya hadithi hii, ingawa ni Qauli ya swahaba je? Inafaa kufanyia kazi hadithi hii; yaani kumsomea maiti Qur'an baada ya kumzika sio uzushi kufanya hivyo? Nimetuma Hadithi kumsomea maiti Qur’an kwamba Ibn Umar alikuwa amelifanya kuwa ni Mustahab kusoma Suwrah Al-Baqarah. Swali langu ni kwamba ikiwa Swahaba huyu amefanya hivyo, je itakuwa ni makosa kufata mwenendo wake?

 

Haya ndiyo maswali nilo nukuu hadithi kwa kiarabu. Nashukuru sana kwa kunisikiliza na ntumai mtanisaidia kwa hilo Inshallah.

 

Wabillah taufiq 

ـ بابُ ما يقولُه بعدَ الدَّفْن

 4/420 وروينا في سنن البيهقي بإسناد حسن؛ أن ابن عمر استحبَّ أن يقرأ على القبر بعد الدفن أوّل سورة البقرة وخاتمتها‏.‏‏(‏ البيهقي 4/56 وقال الحافظ‏:‏ هذا موقوف حسن‏‏‏).‏

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Nadhani kuwa hii ni mada muhimu sana katika maisha yetu ya leo na kwa kuwa ni jambo ambalo linafanyika sana. Kwa minajili hiyo tumeonelea kuwa badala ya kwenda moja kwa moja katika swali lenyewe tuelezee mengi ambayo yatamfaidisha kila mmoja wetu.

 

Mwanzo ni kutazama uongofu wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kuzuru makaburi. Hebu tutazame Hadiyth zifuatazo:

 

1.     Na alikuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pindi alipowekwa maiti katika mwanandani, akisema: "Kwa jina la Allaah na kwa Allaah, na kwa mila ya Rasuli wa Allaah" [Abu Daawuud].

 

 

2.     Ilikuwa ndio ada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapomaliza kuzika akisimama kaburini na husema: "Muombeni Allaah Amsamehe ndugu yenu na Amfanye thabiti kwani sasa hivi anahojiwa" [Abu Daawuud]. Na hii ni Sunnah ambayo imesahauliwa hivi leo au imeachwa na kuletwa mengine ya kumsomea talqiyn

 

 

Katika Hadiyth hizi hakuna kusomwa kwa Suwrah kadhaa na kadhaa, hakusoma yeye wala Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Pia Hadiyth nyingine ni pale alipozuru Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kaburi ya mama yake, alilia na wakalia waliokuwa pamoja naye. Kisha akasema:

 

 

"Nimemtaka idhini Mola wangu Mlezi ili nimuombee msamaha lakini Amekataa. Na nikamtaka idhini nizuru kaburi, Naye akaniruhusu. Hivyo, zuruni makaburi, kwani kufanya hivyo kunawakumbusha mauti" [Muslim].

 

Na katika riwaya nyingine:

 

 

"Kwa hayo ni mawaidha. Kwa hakika, hilo linawafanya muipe nyongo dunia na kuwakumbusha Aakhirah".

 

 

Ni dhahiri kuwa linalofahamika kutoka kwake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kumuombea msamaha, wala sio kusoma Qur-aan. Na hili ndilo lililopokewa na lenye kuingia katika akili. Na inajulikana kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha salaam za kuwatolea waliolala makaburi pindi tunapowazuru. Na miongoni mwazo ni:

 

 

"As-salaam ‘Alaykum ahlad Diyaari minal Muuminiyna wal Muslimiyn, wa inna in shaa Allaahu bikum Laahiquun [Wa Yarhamu Allaahu almustaqdimiyna minna wal musta-khiriyn] – Amani ishuke juu yenu watu wa nyumba hizi miongoni mwa Waumini na Waislamu, tutakutana nanyi, tunamuomba Allaah Atusamehe, sisi na nyinyi." [Na Allaah Awarehemu wa mwanzo (waliotangulia) na wa mwisho (na watakaofuata)] namuomba Allaah Atupe sisi na nyinyi afya njema." [Muslim na Ibn Maajah].

 

 

Hata hivyo, yapo mambo ambayo yanayomfaa maiti na kuandikiwa thawabu hata baada ya kuaga dunia kwake. Hayo ni kama yafuatayo:

 

 

1.     Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Atakapokufa mwanadamu matendo yake yote hukatika ila mambo matatu: Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye manufaa au mtoto mwema atakaye kuombea du’aa" [Muslim].

 

 

2.     Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema tena: "Hakika katika ‘amali njema ambazo zitamfuatia Muumini (baada ya kifo chake) ni mambo yafutayo: Elimu aliyoifundisha na kuieneza; mtoto mwema aliyemuacha au msahafu aliouacha kama mirathi au Msikiti alioujenga au nyumba ya kupumzikia (wanakaa) walioharibikiwa safari, mto aliotengeneza njia yake, au sadaka aliyoitoa kutoka katika mali yake alipokuwa na afya njema na pindi alipokuwa hai na baada ya mauti yake" [Ibn Maajah na Ibn Khuzaymah].

 

 

3.    Maiti anafaidika kwa kutolewa sadaka kwa niaba yake kama alivyopokea [Al-Bukhaariy kuwa kuna mtu alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika mama yangu amefariki, je atafaidika nikimtolea sadaka?" Akasema: "Ndio".

 

 

4.   Maiti anafaidika kwa du’aa za Waislamu na kuwaombea msamaha kwa kauli ya Aliyetukuka:

 

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ...

Na wale waliokuja baada yao wanasema: Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; [Al-Hashr : 10].

 

 

5.     Kumlipia maiti funga, nadhiri na kumhijia kunamnufaisha kwa mujibu wa maelekezo yafuatayo. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Atakayekufa ilhali kaacha deni la funga basi na alipiwe na walii" [al-Bukhaariy na Muslim]. Sa‘d bin ‘Ubaadah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika mama yangu amefariki na aliweka nadhiri". Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Mlipie nadhiri yake au tekeleza nadhiri yake". Imepokewa na Muslim kuwa mwanamke kutoka katika kabila la Khath’am alisema: "Baba yangu ni mzee sana na ana faradhi ya Hijjah ambayo hakuitekeleza naye hawezi kukaa juu ya mgongo wa mnyama". Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: "Mhijie". Ama kuhusu Hijjah inatakiwa kwa mwenye kumhijia mwenziwe awe yeye mwenye ashatekeleza nguzo hiyo.

 

 

Ama kauli za mufassirina kuhusu suala hili ni kuwa hilo halifai kisheria kufanywa. Hebu tutazame baadhi ya kauli zao:

 

 

1.     Tafsiyr Qur-aan al-‘Adhwiym ya Imaam Ibn Kathiyr: Amesema Ibn Kathiyr katika kusherehesha Aayah zifuatazo:

 

وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ ﴿٣٩﴾وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَىٰ ﴿٤٠﴾ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاءَ الْأَوْفَىٰ ﴿٤١﴾

Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi. Na kwamba juhudi yake itakuja kuonekana.  Kisha atalipwa jazaa kamilifu. [An-Najm: 39-41].

 

 

Amesema: “Kama vile madhambi ya mtu hayatobebeshwa mtu mwengine ndivyo namna ambayo ujira wake utakuwa ni wake. Na kwa Aayah hizi tukufu ametoa dalili Imaam ash-Shaafi‘iy na wenye kumfuata kuwa kisomo cha Qur-aan hakimfikii maiti kwani hiyo si katika ‘amali yake wala chumo lake. Na kwa ajili hiyo hakupendekeza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ummah wake wala hakuwahimiza wala hakuwaongoza kwayo kwa nasw (andiko). Na wala hilo halikupokewa kutoka Swahaba yeyote (Radhiya Allaahu ‘anhum), na lau ingekuwa ni kheri basi wangetutangulia”. Akaendelea kwa kutoa Hadiyth ifuatayo: "Atakapokufa mwanadamu matendo yake yote hukatika ila mambo matatu: Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye manufaa au mtoto mwema atakayekuombea du’aa" [Muslim]. Kisha akasema: “Kwa hakika mambo yote haya matatu ni katika aliyoyafanya mwenyewe”.

 

 

2.     Tafsiyr Fat-hul Qadiyr ya ash-Shawakaaniy: Amesema yafuatayo katika kusherehesha Aayah ya 39 ya Suratun Najm: "Na maana yake ni kuwa hatopata ila ujira wa aliyofanya na jazaa ya ‘amali yake wala hatonufaishwa mtu na ‘amali ya mwenziwe".

 

 

3.     Tafsiyr al-Mannaar: Baada ya utafiti wa kina kuhusiana na Aayah ya 164 ya Suwrah Al-An‘aam (6), amesema: “Hakika kila linalopitika katika ada kwa kusoma Qur-aan na adhkaar, na kumpatia hadiya ya thawabu zake maiti na kuwaajiri wasomaji na kushika wakfu juu ya hayo, ni uzushi usiokuwa ndani ya sheria. Na hakika Hadiyth ya kusoma Suwrah Yaasiyn (36) kwa maiti si sahihi. Na wala haisihi katika mlango huu Hadiyth yoyote kama alivyosema hivyo Muhaddith ad-Daaraqutwniy. Na fahamu kuwa iliyokuwa mashuhuri kwa mabedui na waliohudhuria kwa kusoma Suratul Faatihah kwa ajili ya maiti haikupokewa kwa Hadiyth sahihi wala dhaifu. Kwa hiyo, hiyo ni bid‘ah inayokwenda kinyume na yaliyotangulia. Na ufupisho wa kauli ni kuwa suala hili ni katika mambo ya Ki-‘Ibaadah, ambayo ni wajibu kwetu kusimama kwenye andiko, Kitabu, Sunnah na ‘amali ya watangu wema wa mwanzo. Hakika tunafahamu kuwa msingi uliowekwa katika nasw za Qur-aan zilizo wazi na Hadiyth sahihi ni kuwa watu hawalipwi Akhera ila kwa amali zao:

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ وَاخْشَوْا يَوْمًا لَّا يَجْزِي وَالِدٌ عَن وَلَدِهِ وَلَا مَوْلُودٌ هُوَ جَازٍ عَن وَالِدِهِ شَيْئًا ۚ 

Enyi watu! Mcheni Rabb wenu, na iogopeni Siku ambayo mzazi hatomfaa mwanawe na wala mwana hatomfaa mzazi wake chochote. [Luqmaan : 33].

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwajulisha watu wake kwa amri hiyo itokayo kwa Rabb wake Mlezi: ‘Fanyeni ‘amali, kwani mimi sitoweza kuwafaa na lolote kwa Allaah’ [al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Ama kauli za Imamu (Abu Haniyfah, Maalik, ash-Shaafi‘iy na Ahmad) wote kwa umoja wao wamesema kisomo cha Qur-aan hakimfikii maiti. Na Faqiyh, Imaam Mulla ‘Aliy al-Qaari’ al-Hanafiy amesema: "Kisha kisomo cha Qur-aan kaburini ni jambo linalochukiza kwa madhehebu ya Abu Haniyfah, Maalik na Ahmad kwani ni uzushi ambao haukupatikana katika Sunnah".

 

 

Ama ile kauli iliyopokewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwa aliusiya asomewe Aayah za mwanzo za Suwra Al-Baqarah na Aayah za mwisho za Suwrah Al-Baqarah (2) kwenye kaburi lake. Hiyo ni athar shaadh ambayo isnadi yake si sahihi. Na kwa hilo hakuafikiwa na yeyote miongoni mwa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Na pia yale yaliyopokewa katika kusoma Al-Faatihah, Al-Baqarah, Al-Ikhlaasw, Al-Falaq na An-Naas, At-Takaathur na Al-Kaafiruun na kuwapatia hadiya maiti ni batili zinazokwenda kinyume na kauli za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na matendo ya Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

 

Twatumai kuwa maelezo haya yako wazi kabisa na yatatusaidia kwa kiasi kikubwa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share