Kuweka Nywele Za Rasta Nini Hukmu Yake?

 

Kuweka Nywele Za Rasta Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Assalaam Alaykum,

 

Poleni na kazi za hapa na pale katika suala zima la kusukuma gurudumu la uislam. Nauliza juu ya suala zima la ufugaji wa rasta km mtindo kwa muislam, je kuna uhalali wowote juu ya hili?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kuweka rasta ni njia ambayo inatumiwa na Rastafarians wenye itikadi tofauti kukiwemo ushirkina. Kwa hiyo, hao wenye itikadi hiyo wanafanya mengi ya kikafiri hivyo inahitajika nasi tuhalifu mambo yao, la kuweka rasta likiwa ni mojawapo kwa kwenda kinyume na unadhifu wa Uislamu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kujifananisha na watu yu pamoja na wao”. Na Imaam an-Nawawiy naye ana mlango aliouita: “Mlango Kukatazwa Kujifananisha na Shaytwaan na Makafiri.”

 

Kwa hiyo, haifai kwa Muislamu mwenye kumuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na mwenye kuipenda Dini yake na kila kilichokuja pamoja na Dini hii miongoni mwa mafunzo mbalimbali ya namna Muislamu anavyopaswa kujiweka, kuvaa, unadhifu, ufugaji nywele na utunzaji wake, ufugaji ndevu na mengi mengine mazuri yaliyoletwa na Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Kuweka rasta ni njia mojawapo ya kujifananisha na Rastafarian, na hawezi mtu kuwa hapo hapo ni Muislamu na hapo hapo anataka kuwa Rastafarian.

 

Na polepole mtu atawaiga hao wasio Waislamu kwa mwendo mmoja hadi mwengine, ataanza na nywele, kisha atafuatia na kujizuia kula nyama, kisha atafuatia na kuvuta bangi na mengi mengine ambayo yanapingana na kwenda kinyume na Uislamu.

 

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Nini Hukumu Ya Nywele Za Bandia?

 

Hukmu Ya Mtu Kuswali Na Kaweka Nywele Za Bandia

 

Kuvaa Nywele Za Bandia Kufunika Nywele Turkey Kwa Sababu Ya Kukatazwa Hijaab

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share