Jinsi Ya Kumsilimisha Mtu Kuingia Uislamu

 

SWALI:

Assalam alikum warahma tullahi taala wabarakatu,

Ni nini unatakiwa kufanya ili umsilimishe mtu?... Naombeni jibu, kwasababu nina rafiki yangu ambaye ananiya ya kuingia kwenye uislamu ila sina uhakika wa taratibu ya kusilimisha mtu asiye muislamu. Shukran nategemea jibu hivi karibuni... wabillahi tauri

 

 


 

JIBU:

 

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Kumsilimisha mtu ni jambo jepesi kabisa ila baada ya kumsilimisha kuna ya muhimu ya kuzingatia ambayo tunakuwekea maelezo chini ya hizi taratibu za kumsilimisha.


 
Kwanza kabisa kama utaweza kumpata mwenye kujua Dini ni bora kwani ataweza pia kumuongoza mtu  huyo na kumpa mawaidha na maelekezo muhimu baada ya kumsilimisha. Ama ikiwa hayupo mwenye kuijua Dini vizuri, basi aliyepo hata wewe unaweza kumslimisha kwa kutekeleza yafuatayo:

 

  1. Utamtaka akiri Shahaada kwa kutamka wewe maneno haya kidogo kidogo ili aweze kukufuata, naye ayatamke nyuma yako, kwanza kwa Kiarabu kisha kwa Kis.

 

Ash-hadu an laa ilaaha illa-Allaah, wa ashhadu anna Muhammadar Rasuulu-Allaah.

  

(Nakiri na kutamka kuwa hapana apasaye kwa dhati kuabudiwa ila Allaah, na nakiri kuwa Muhammad ni Mjumbe Wake)

 

(Haya tuliyopigia mstari unaweza kumtaka atamke ingawa si lazima sana, hutumika ikiwa mtu alikuwa Mkiristo na anaamini kuwa 'Iysa (Jesus) ni mungu au mwana wa mungu). Wa ash-hadu anna ‘Iysa Rasuulu-Allaah  

(Na nakiri kuwa 'Iysa (Yesu) ni Mjumbe wa Allaah na si mungu au mwana wa mungu.'

 

Akitamka yote hayo hapo juu basi tayari ameshakuwa Muislamu.

 

  1. Ikiwa ni mwanamke akate kucha zake, apunguze au anyoe nywele za kwapani na sehemu zake za siri.  

 

  1. Ikiwa ni mwanaume akate kucha zake, apunguze au anyoe nywele za kwapani na sehemu zake za siri, anyoe nywele za kichwani na kisha baadaye akatahiriwe (Jando) kama bado hajatahiriwa (si lazima siku hiyo hiyo),  kutahiri ni Sunnah ya Mitume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) kama ilivyo dalili katika Hadiyth ifuatayo:

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) alimuamrisha Kafiri mwanamume aliyesilimu: ((Nyoa nywele za ukafiri na fanya tohara [jando])). [Abu Daawuud, na imepewa daraja ya Hasan na Shaykh Al-Albaaniy]

 

Tanbihi: Nywele za kwapani na sehemu za siri zisikae zaidi ya siku arubaini bila ya kunyolewa au kupunguzwa kwa Waislam wote.

 

  1. Kuoga (ghusul) na kuvaa nguo safi kwa maana zisizokuwa na najsi yoyote kama mkojo, kinyaa au mate ya mbwa.

 

  1. Afunzwe kuswali, na atekeleze Swalaah tano bila ya kuziacha

 

  1. Unaweza  kumshauri akachagua jina lolote zuri la Kiislam akalitumia badala ya kina lake la Kikafiri (ingawa si lazima abadili jina lake, ila ni vizuri ili atambulike kuwa ni Muislam). Majina mazuri ni haya hapa:
     
    Fiqh Ya Kuwaita Majina Watoto

 


 

Mambo muhimu kutekeleza baada ya kumsimilisha Muislamu
 

 

Usimuache baada ya hapo, bali mpe vitabu vya Dini, mfundishe Dini vizuri, ikiwa wewe hujui mtafutie Mwalimu japo umlipe aweze kumfundisha Uislam. Makosa makubwa yanafanywa sana na Waislam, ni kuwa baada ya kumsilimisha mtu humwacha akaenda zake na hawamfuatilizii wala hawamsaidii kumfundisha Dini wala kujua kama anaswali, anafunga n.k. Jaribu kumsaidia kwa hali na mali kadiri uwezavyo ili kumpa moyo na kumuonyesha undugu wa Kiislamu.
 
Pia makosa makubwa yanatokea kwa kuwa wale wanaowasilimisha watu au kusababisha wasilimu, wao wenyewe hawatekelezi mafundisho ya Dini, hawaswali, hawana tabia njema za Kiislam na hata hawaijui Dini yao wenyewe. Jambo hilo huja kuwachanganya sana wanaosilimu, kwani wanakuta Uislamu unasema vingine na Waislamu wanafanya vingine!
 
Tunatumai ndugu yetu humo katika tabia hizo. Na ikiwa ni mtu ambaye hufuati mafunzo ya dini yako kamili, basi hukuchelewa sana, tunakunasihi, uanze kutekeleza na kujifunza kwa kusoma au kuhudhuria madarsa na mihadhara ya Dini n.k. kwani usipofanya hivyo ujue kuwa mtu huyu unayemsilimisha atasilimu jina tu lakini kivitendo hatopata mafunzo na mifano kutoka kwako atabaki kama alivyokuwa katika ukafiri wake kwani atakuwa anakutegemea sana wewe khaswa kwa kupata mafunzo ya dini yake.

    Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share