Mashairi: Tufanye Mema Kwa Wingi, Siku Kumi Dhul-Hijjah

Tufanye Mema Kwa Wingi Siku Kumi Za Dhul-Hijjah

Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

www.alhidaaya.com

Salaam  zangu za dhati, ninazirusha angani,

Ziwafikie umati, kila pembe duniani,

Naomba kila wakati, tujumuike peponi,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Siku kumi za awali, ni siku zenye thamani,

Anazipenda Jalali, zipo kwenye Qur-aani,

Tujitahidi kikweli, kila dakika ombeni,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Watu wanaposimama, Arafati uwanjani,

Shetani anainama, mwenye uso wa huzuni,

Anahisi amekwama, ameshindwa hadharani,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Siku hiyo ni ya tisa, ni siku kubwa oneni,

Tuzingatie kabisa, dua ziwe mdomoni,

Epukana na makosa, na ugomvi mitaani,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Saumu ya hiyo siku, isiwakose jamani,

Malipo yake makuu, akhera kwenye mizani,

Siku ya kumi sikukuu, Eid-ul-Adh'ha nchini,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Mwaga damu ukiweza, ukachinje hayawani,

Mungu Inampendeza, damu kumwagika chini,

Kwa Jina Lake Muweza, chinja uwe furahani,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Nyama wape masikini, pamoja na majirani,

Fungu lingine yakini, ni lako na wa nyumbani,

Ni Sunnah ilobaini, toka zama za zamani,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Ng’ombe, kondoo na mbuzi, ngamia, zote chinjeni,

Kwa Jina Lake Mwenyezi, usisite asilani,

Kama kuchinja huwezi, Umshukuru Manani,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Mnyama awe timamu, hana kilema mwilini,

Awe mkubwa makamu, uchunguze kwa makini,

Alichinja Ibrahimu, Mtume wa Rahmani,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Ndoto ilithibitika, kaota usingizini,

Kaambiwa na Rabbuka, Chinja mwana kwa imani,

Kumchinja alitaka, mwanawe kisu shingoni,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Hapo kaja Jibrili, na kondoo mkononi,

Ikawa ndio badili, ya mwana wa Muhisani,

Kwa hivyo hiyo dalili, ya kuchinja ikhwani,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Kafatwa na mashetani, wambadili maoni,

Karusha mawe hewani, kuwapiga kuwalaani,

Na wakashindwa mwishoni, kumshawishi moyoni,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Na mpaka leo tazama, Mahujaji Waumini,

Wamewekewa alama, kama kupiga shetani,

Mpaka siku ya Qiyama, shetani tutamlaani,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Hapa ndio kaditama, nimeshafika mwishoni,

Na mwezi umeandama, amewasili mgeni,

Labbayka Allaahumma, Labbayka laa Shariyka Lak,

Tufanye mema kwa wingi, siku kumi Dhul Hijjah.

Share