Mashairi: Mwaka Mpya Wa Kiislamu

                   

                     Mwaka Mpya Wa Kiislamu                

                     Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

Alhidaaya.com

 

 

                

 

Salaam nazipeleka, ziwafike Afrika,

Mwaka mpya umefika, utapita kwa haraka,

Tupate kufaidika, lazima dini kushika,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Tuzidi kuelimika, tupate kuerevuka,

Akili kunawirika, na macho yatafunguka,

Adui atashtuka, na hawezi kutucheka,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Sherehe haikufanyika, mwaka mpya ukifika,

Wala haukutajika, na wala kuadhimika,

Lakini ninaandika, mema yapate tendeka,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Wengi tunashughulika, kutwa tunahangaika,

Kila kitu tunataka, upesi kutajirika,

Kweli tumeghafilika, akhera kuikumbuka,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Tupo mbioni hakika, kila pembe tunafika,

Na shetani hakuchoka, na sisi kila dakika,

Nia yake anataka, motoni kutupachika,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Rahisi kumuepuka, dua inapoombeka,

Nyumbani tunapotoka, kuna kinga husomeka,

Apate kutuepuka, shetani alolaanika,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Na Mola Ataridhika, mema yanapotendeka,

Mazuri yatatufika, na watu kuneemeka,

Na shida zitaondoka, na madhambi kufutika,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Tusisahau sadaka, wenye shida kuwafika,

Wapate kufurahika, Mola hivyo Anataka,

Na nia kusafishika, rehema itateremka,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Mola Anaghadhibika, maasi yakifanyika,

Tunapovuka mipaka, tabia kuharibika,

Mwisho wake kudondoka, halafu kufilisika,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Tupate kunusurika, Tumuombe Mtukuka,

Tupate kuhifadhika, na tupate kuokoka,

Wabaya kuwaepuka, na mbali kuwatoroka,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Jogoo ameshawika, lini jamaa tutamka,

Wakati unatuvuka, na lini tutazinduka,

Hapa mwisho nimefika, inatosha kuandika,

Mwaka mpya umefika, tuzidi kuelimika.

 

 

Share