Kumsomea Maiti Surat Yaasiyn Anapooshwa, Au Akishazikwa Pamoja Na Du'aa Inafaa?

 

Kumsomea Maiti Surat Yaasiyn Anapooshwa, Au Akishazikwa Pamoja Na Du'aa Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI LA KWANZA:

 

Assalaamu alaikum warrahmatullahi wabarakatu.

Swala langu ni hili:Maiti akishazikwa inafaa asomewe sura-Yasin pamoja na dhikiri au kumuombea dua tu na watu waondoke?
 

Jazaakumullahu kheiran.

 

 

SWALI LA PILI:

 

Assalamu alekum,

 

Tunashukuru kututoa kizani na hasa mambo ya bidaa ambayo wengi tulikuwa hatujui tunafuata tu. 

 

Swali langu ni je, maiti anapokata roho au anapokoshwa na kukafiniwa inafaa kumsomea Yaasiyn? Na pia pale akishazikwa watu hubakia kaburini kumsoema Yasin na duaa kwa pamoja, je kuna dalili yoyote kuhusu jambo hili? 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Imekuwa ni ada katika jamii yetu kumsomea mtu anapokata roho au pale anapooshwa au akishazikwa Suwrah Yaasiyn na du'aa kwa pamoja. Tutambue kwamba ibada yoyote inayotendwa lazima ipatikane dalili, bila ya kwayo, huwa ni kitendo kisichokuwa na thamani mbele ya Allaah, wala hakimfai maiti kwa lolote lile!

 

 

Suwrah Yaasiyn hasa imekuwa maarufu kusomewa maiti. Maiti anapokata roho au akishafariki, na wengi wakiitumia dalili ya Hadiyth hii ambayo sio sahihi:

 

"Someni Yaasiyn kwa maiti wenu" [Abu Daawuud]

 

 

("Maiti wenu' hapo wengine wamefahamu kuwa ni wale wanaokata roho, na wengine wamefahamu kuwa ni wale tayari waliokwishakufa) Ndio maana utakuta mtu anapotaka kukata roho watu hukimbilia kumsomea Yaasiyn, na wengine baada ya kumzika humsomea maiti wao Yaasiyn kwa ufahamu wao wa Hadiyth hiyo ambayo ni dhaifu. Imaam An-Nawawiy, Ibn Hajar, Adh-Dhahabiy, Ibn Al-Qattwaan, Al-Albaaniy na wengineo wamesema Hadiyth hiyo ni dhaifu.

 

Anapofariki mja hakuna tena limfaalo ila mambo matatu kama ilivyo dalili katika Hadiyth:

 

"Anapofariki mwanaadamu ‘amali zake zote hukatika isipokuwa kwa mambo matatu: Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye manufaa na mtoto mwema mwenye kumuombea du’aa (mzazi/wazazi anapofariki)".  [Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah].

 

 

Na katika Suwrah Yaasiyn yenyewe kuna ushahidi kwamba Qur-aan ni kwa ajili ya kuwaonya walio hai na sio waliokwishafariki. Sasa vipi iwe kinyume chake?

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ ﴿٦٩﴾لِّيُنذِرَ مَن كَانَ حَيًّا وَيَحِقَّ الْقَوْلُ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٧٠﴾

Na hatukumfunza (Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) mashairi, na wala haipasi kwake, hii si chochote isipokuwa ni ukumbusho na Qur-aan bayana. Ili imuonye yule aliyekuwa hai na neno lihakikike juu ya makafiri. [Yaasiyn: 69-70]

 

 

Pia kumsomea du'aa kwa pamoja sio jambo lilotendeka katika Sunnah, achilia mbali kumsomea maiti, hata kukusanyika kusoma du'aa pamoja kwa ajili ya jambo lolote lile haina dalili.

 

 

Hadiyth mbalimbali ambazo ima ni dhaifu au za kutungwa inazotumiwa sana na watu kuonyesha au kuthibitisha fadhila za Suwrah Yaasiyn ni hizi zifuatazo:

 

Kutoka kwa Anas Bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Atakayeingia makaburini na akasoma Suwrah Yaasiyn atawafanyia wepesi (maiti) siku ya masiku, na ataandikiwa mema idadi ya walio humo makubirini." Imesimuliwa na As-Sakhaawiy . Imechambuliwa kuwa ni Hadiyth ya kutungwa kutoka katika kitabu cha 'Silsilatul Ahaadiyth Dhwa'iyfah' /1246

 

kutoka kwa Anas Bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): "Kila kitu kina moyo, na moyo wa Qur-aan ni Suwrah Yaasiyn, atakayesoma Yaasiyn ataandikiwa thawabu za kusoma Qur-aan yote mara kumi." Imesimuliwa na Adh-Dhahabiy. -Imechambuliwa kuwa ni Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'At Targhiyb wat-Tarhiyb' /885

 

"Atakayesoma Yaasiyn kwa kutaka Ridhaa ya Allaah ataghufuriwa madhambi yaliyomtangulia, basi isomeni kwa maiti wenu."  Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'Aj Jami'i Asw-Swaghyr'/5785.

 

"Atakayesoma Yaasiyn katikati ya mchana atakidhiwa haja yake" Hadiyth dhaifu kutoka katika kitabu 'Mishkaat Al-Maswaabiyh'/2118.

 

 

Naye Imaam Ad-Daaraqutwniy kasema hakuna katika fadhila za Surah Yaasin Hadiyth yoyote iliyosihi.

 

 

Bali lililo sahihi kusomewa anayekaribia kufa ni kauli ya "Laa Illaaha Illa Allaah". Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Yule atakayekuwa neno lake la mwisho ni Laa ilaaha illa Allaah ataingia Peponi". (Ahmad na Abu Daawuud).

 

Bonyeza viungo vifuatavyo ambavyo vinatoa maelezo zaidi kuhusu mas-ala ya Suwrah Yaasiyn na kumsomea maiti Qur-aan:

 

 

Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Duaa Kwa Pamoja

 

Kumsomea Qur-aan Maiti Akishazikwa

 

Fadhila Za Surat Yaasiyn Na Al-An'aam

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share