Kutumia Vidole Vya Mikono Miwili Kuleta Tasbihi Inafaa?

 

Kutumia Vidole Vya Mikono Miwili Kuleta Tasbihi Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum warahmatullah. Amma baada ya maamkizi mema, namshukuru Allaah kwa kutujaliya mtandao kama huu na Awapatie tawfiq wanao fanya kazi hii. Swala langu ni kuwa kuleta tasbih/ dhikr kwa mikono yote miwili ni sawa? Kunao dalili la kulisisitiza jambo kama hili? Jazakallahu kheir. Assalam aleikum.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika dhikr inatakiwa iletwe kwa njia ambayo ametufunza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi aalihi wa sallam). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi aalihi wa sallam) alikuwa akileta dhikr na akihesabu kwa kutumia mkono wa kuume peke yake:

 

'Abdullaah bin 'Amr bin al-'Aasw (Radhwiya Allaahu anhuma) anasimulia, "Nilimuona Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akihesabu kumsabihi Allaah na vidole vya mkono wake wa kuume" [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah].  

 

 

Kwa hiyo ili kufuata Sunnah inabidi nasi tutumie mkono huo.

 

 

Na utaratibu mzuri wa kutumia vidole kama tulivyopata kutoka kwa Wanachuoni walioelewa masuala hayo ya kutumia vidole, wanasema ni kutumia matumbo ya vidole karibu na kucha kuhesabia na si ile mistari mitatu ya kila kidole kama ilivyozoeleka na wengi. Lakini atakayefanya kwa njia zote hizo maadam anatumia vidole vyake, basi katimiza Sunnah na ana ujira mkubwa kwa hilo.

 

 

Na haipendezi kutumia mkono wa kushoto kwa kuhesabia dhikr unazofanya.

 

 

Na mambo mema yote yanafanywa kwa kutumia mkono wa kuume. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi aalihi wa sallam) alikuwa akipenda kufanya mambo yake yote kwa mkono wa kulia. Anasema Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa):

 

"Alikuwa akipenda Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuanza kuutumia mkono wa kulia wakati akivaa viatu vyake, na kujichana kwake, na katika kujitwaharisha kwake, na katika kutenda mambo yake yote." [Al-Bukhaariy Na Muslim].

 

 

Kutumia Tasbihi Katika Kumdhukuru Allaah Inafaa?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share