Talaka Ya Mara Tatu Inasihi?

 

SWALI:

Swali langu kama mwanaume ameandika talaqa kwenye karatasi akasema namuacha mke wangu talaqa tatu je zinahesabiwa talaqa tatu au moja?

 


 

JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Shukrani sana kwa dada yetu aliyeuliza swali hili. Na hakika hili ni tatizo kubwa sana kwa jamii zetu za Waislamu katika nchi tofauti. Hii yote inarudi kwetu sisi kwa kupuuza masomo ya Dini yetu tukufu na matatizo haya yataendelea mpaka tutakapoamua kurudi kwa Dini yetu katika kila mambo yetu.

Talaka ya aina hii katika sheria inaitwa Twalaqul Bidi‘iy (Talaka ya Kuzuliwa) kwani huwa imekwenda kinyume na sheria tukufu ya Kiislamu. Na hii ni ima kumpatia talaka mke wako akiwa katika damu ya hedhi, nifasi au talaka tatu kwa mara moja au sehemu moja.

Wanazuoni wa Kiislamu wametofautiana kama talaka tatu mara moja zinahesabiwa kuwa ni tatu au ni moja. Hii ni kwa sababu kila kundi limetoa ushahidi kwa rai zao. Lakini kauli yenye nguvu zaidi ni kuwa mume anayetoa talaka tatu kwa mara moja inahesabiwa kuwa ni talaka moja lakini atakuwa amefanya makosa na madhambi katika tendo lake hilo na inabidi aombe msamaha.

Wakati mmoja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipashwa habari ya kuwa kuna mtu aliyetowa talaka tatu kwa mara moja. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikasirika sana na kishaa akasema: “Mnachezea Kitabu cha Allah, nami bado nipo baina yenu” (An-Nasai, na akasema Ibn Kathiir kuwa Isnadi yake ni Nzuri).

Na alikuwa ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) akiletewa mtu ambaye ametoa talaka tatu kwa mara moja akimpiga viboko (Ibn Abi Shaybah).

Na katika mas-ala haya Allah ametuambia: “T'alaka ni mara mbili” (2: 229).

Hii inamaanisha moja baada ya nyingine na wala siyo kuzitoa kwa wakati mmoja. Sayyid Sabiq katika Fiqhis Sunnah anasema kuwa hii ndiyo iliyokuwa njia iliyofuatwa wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Abubakr, ‘Umar na Makhalifa wengine (Radhiya Allaahu 'anhum) kabla kubadilishwa.

Na hakika inaonyeshwa wazi wazi wakati wa Sheikh Ibn Taymiyah alipotoa rai hii alipingwa sana na wanazuoni wa wakati wake lakini wanazuoni wa sasa wameirudia kauli hiyo ambayo ndiyo yenye nguvu.

Kwa manufaa zaidi bonyeza viungo vifuatavyo :

 

Talaka Tatu Pamoja Inakubalika? Mume Hatimizi Zamu Kisha Ametoa Talaka Mara Tatu Kwa Pamoja

Mas-ala Ya Talaka Mbali Mbali

Talaka Ziko Aina Ngapi Na Wakati Gani Zinasihi?

 

Na Allaah Anajua zaidi. 

 

 

Share